Habari za Punde

CWT Iringa Vijijini Wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa Kuwapandisha Madaraja.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Hassan Moyo akiongea na kuzungumza na Walimu wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Walimu wa Wilaya hiyo 
Mwenyekiti wa CWT Iringa Vijijini mwalimu Saimon Mnyawami Akizungumza wakati wa mafunzo kwa walimu wa wilaya ya Iringa vijijini akiwa sambamba na viongozi wengine.
Baadhi ya walimu waliohudhuria nafunzo hayo wakiwa na furaha tele

Na Fredy Mgunda,Iringa.

CHAMA cha walimu wilaya ya Iringa vijijini (CWT) wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha madaraja na kuongeza ajira za walimu kwa kipindi kifupi ambacho yupo madarakani.


Akizungumza wakati wa mafunzo kwa walimu wa wilaya ya Iringa vijijini,Mwenyekiti wa CWT Iringa Vijijini mwalimu Saimon Mnyawami alisema kuwa walimu wanafura kubwa kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawajali kwa kuwapandisha madaraja ambayo yanasaidia kuongezeka kwa mshahara.


Alisema kuwa walimu wote 1032 waliopandishwa madaraja wamesharekebishwa mishahara tangu mwezi wa sita na mwezi wa saba na wapo tayari kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kila jambo hata akisema atagombea urais  2025 basi watamuunga mkono.


Mnyawami alisema kuwa walimu wote 2244 wa wilaya ya Iringa vijijini watashiriki vilivyo kutoa elimu ya sensa ambayo itafanyika mwakani kwa kuwa zoezi la sensa  litasaidia katika mipango ya serikali kwasababu watakuwa wanajua idadi ya wananchi wa maeneo husika.


Alisema kuwa zoezi la sensa ni muhimu sana kwa taifa kujua idadi ya wakazi kwa ajili ya kupanga mipango ya kuleta maendeleo kwa wananchi hivyo jukumu la walimu kumuunga mgono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufanikisha zoezi hilo kwa asilimia 100.


Aidha Mnyawami alikemea vitendo vya baadhi ya walimu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi jambo ambalo linachafua taswira ya kada hiyo ya walimu hivyo walimu wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi yao.


Alisema kuwa walimu wanapaswa kuendelea kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii ambazo wanaishi nazo huku ili kuwa na kizazi ambacho kitakuwa na maadili bora nakutomeza kabisa maswala yote ya ukatili wa kijinsia.


Mnyawami alisema walimu wanatakiwa kuendelea kuwa na maadili bora ili kuwasaidia wananchi wengine kuiga mfano wao kwa namna ya kufanya kazi kwa kujituma na kulijenga taifa kiuchumi na kielimu.


Alisema kuwa rushwa ni adui wa maendeleo ya wananchi wote hivyo walimu wanatakiwa kuwa matari wa mbele kuhakikisha wanapinga vitendo vyote vyenye viashiria vya rushwa.


Mnyawami alimalizia kwa kumuomba mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo kufikisha ujumbe wao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa walimu wa wilaya ya Iringa vijijini wanaiunga mkono serikali ya awamu ya sita kutokana na kazi ambayo wanaifanya.


Akifungua mafunzo kwa waalimu wawakilishi mahali pa kazi yanayoendeshwa na chama cha Waalimu Wilaya ya Iringa Vijijini (CWT),Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka walimu kuwa mabalozi wa kukemea vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi yao ikiwemo kujihusisha kingono na wanafunzi kwani tabia hiyo inadharirisha taaluma yao.


Moyo alisema kuwa waalimu wenye maadili ni lazima wajikite kwenye uzalendo na uadilifu ili kuwa mfano bora kwa jamii.Alisisitiza kuwa viongozi wa CWT wanatakiwa kuweka mikakati ya kuwabaini waalimu wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi ili kukomesha tabia hiyo ya unyanyasaji na ukatili unaokatisha ndoto za wanafunzi hasa wa kike.


Moyo alisema kuwa ni aibu kusikia mwalim ana mahusiano ya ki ngono na mwanafunzi jambo hilo limekuwa likiitia doa kada ya ualimu kwa vitendo amvyo  vinafanywa na baadhi ya walimu kwa wanafunzi.


“Kama wewe ni kidume wa ukweli nenda kwenye bar na vilabuni katafute wanawake kule mbona wapo wengi kwanini ukimbilie kwa wanafunzi na kuwaharibia ndoto zao”alisema Moyo alisisitiza kuwa waalimu wote wanatakiwa kuwa mfano bora wa kuigwa na jamii kwa  kukemea vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili katika jamii.


Aidha Moyo alizungumzia changamoto za maslahi kwa waalimu na kuwahakikishia kuwa Serikali inazitambua na inazifanyia kazi kwa awamu


Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Chama cha waalimu CWT yamelenga kuwajengea uwezo waalimu wa wakilishi kutoka shule zote za wilaya ya Iringa juu ya Masuala ya Sheria za kazi, wajibu wa waalimu na namna bora ya kushughulikia migogoro mahala pa kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.