Na Mwandishi Wetu, HESLB DAR-ES-SALAAM
BODI
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa muda wa siku nne kuanzia
Oktoba 4-7, mwaka huu kwa wanafunzi 2,982 walioomba mikopo kwa mwaka 2021/2022 kufanya
marekebisho ili kukamilisha taratibu za maombi yao.
Ili
kupata taarifa za kina kuhusu marekebisho hayo, waombaji husika wameshauriwa
kutembelea akaunti zao walizotumia kuomba mkopo kwa njia ya mtandao maarufu
kama SIPA-Student’s Individual Permanent Account (SIPA).
Akizungumza
katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mkurugenzi wa
Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB, Dkt. Veronica Nyahende alisema mara baada ya
kukamilika kwa hatua hiyo ya marekebisho, HESLB itaanza kuwapangia mikopo
wanafunzi wahitaji.
“Katika
uhakiki wa maombi tumebaini waombaji 2,982 fomu zao zina kasoro. Tumetoa
muda wa siku nne, na baada ya hatua hiyo kukamilika tutaanza mchakato wa
kupanga mikopo kwa wanafunzi wenye sifa na uhitaji”, alisema Dkt. Nyahende.
Kwa
mujibu wa Dkt. Nyahende waombaji pia watapaswa kutembelea akaunti za SIPA ili
kupata taarifa za mikopo watakayopangiwa na HESLB baadaye mwezi huu.
Hadi
kufikia Septemba 30, mwaka huu, HESLB ilikuwa imepokea maombi 88,688 na kati ya
maombi hayo; 85,706 yalikuwa kamilifu na 2,982 yalitakiwa kufanyiwa
marekebisho.
Dkt.
Nyahende aliongeza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha fedha za
mikopo ya wanafunzi zinalipwa kabla ya vyuo vya elimu ya juu kuanza kufunguliwa
kuanzia Oktoba 25 mwaka huu.
Katika
mwaka wa masomo 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha TZS 570 Bilioni
kwa ajili ya bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 162,000 wakiwemo
wanafunzi 62,000 wa mwaka wa kwanza na 98,000 wanaoendelea na masomo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment