Habari za Punde

Kamati ya Bunge ya Kudumu Inayoshughulikia Masuala ya Ukimwi Kifua Kikuu,Dawa za Kulevya Yapongezwa kwa Ushirikiano.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inashuhulikia masuala ya ukimwi, kifua kikuu, madawa ya kulevya waliofika Afisini kwake Vuga kubadiliana nae mawazo.

Na.Kassim Abdi. OMPR. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Kamati ya kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya Ukimwi, Kifua kikuu, Madawa ya kulevya pamoja na maradhi yasioambukiza kwa ushirikiano wake kwa serikali ya mapinduzi Zanzibar.

Mhe. Hemed alieleza hayo katika kikao maalum kilichowakutanisha wajumbe wa kamati hiyo waliofika afisini kwake vuga jijini Zanzibar kwa lengo la kubadilishana nae mawazo.

Alieleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafarijika kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa kamati hiyo, kwa ushirikiano wa pamoja na viongozi wake ambapo kwa kiasi kikubwa imesaidia kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya.

Alibainisha kwamba, kutokana na Zanzibar kuwa nchi ya visiwa, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upitishaji wa madawa ya kulevya, kutokana na uwepo wa bandari nyingi zisizokuwa rasmi, zinazotumiwa na wahalifu wa vitendo hivyo.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais alisema kutokana na kadhia hiyo ya uwingizwaji wa madawa ya kulevya, imepeleka Zanzibar kuathiriwa kutokana na vijana kujiingiza katika wimbo hilo, hali inayosababisha kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Alieleza, kutokana na ukubwa wa jeografia ya Tanzania utaratibu wa kubadilishana taarifa kwa pande mbili hizo utasaidia kudhibiti uhalifu wa vitendo hivyo kwa namna moja au nyengine.

Katika hatua nyengine, Makamu wa Pili wa Rais aliwambia wajumbe wa kamati hiyo ya kudumu ya Bunge kuwa serikali haitokuwa na muhali na kiongozi yoyote atakaebainika kujihusha na vitendo vya dawa za kulevya ambapo kupitia baraza lijalo serikali inatarajia kufanya mabadiliko ya sheria ili kuipa meno Zaidi ya kiutendaji tume ya kitaifa ya uratibu na udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar.

Nae, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambae pia ni Mbunge wa Viti maalum Mhe. Fatma Hassan Taufiq alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa kamati hiyo imeamua kufanya ziara yake  Zanzibar  kwa lengo kujifunza hatua bora zilizochukuliwa na serikali ya mapinduzi Zanzibar katika kukabiliana na masuala mbali mbali yanayohusiana na kamati hiyo.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Fatma aliishauri serikali kuangalia namna ya kuliratibu suala la maradhi yasioambukiza kutokana na kuisababishia serikali kubeba gharama kubwa ya matibabu kutokana na magonjwa hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.