Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikata utepe
kuzindua josho la kuogeshea mifugo lenye uwezo wa kuhudumia mifugo 8,327 lililojengwa
katika Kijiji cha Nghambi ikiwa ni moja ya shughuli zinazotekelezwa na Mradi wa
kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini ulipo
chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na unatekelezwa katika Wilaya tano nchini
ambazo ni Mpwapwa, Mvomero, Kishapu, Simanjiro na Kaskazini - A.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipata maelezo kuhusu
hatua za uchimbaji wa visima vitatu kwenye vijiji vya Mbugani, Ngh’ambi na Kiegea
katika Wilaya ya Mpwapwa. Waziri Jafo ametembelea Wilaya ya Mpwapwa leo tarehe
23/12/2021 kukagua shughuli za mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa
kutumia mifumo ikolojia vijijini, ambapo kuna shughuli za uchimbaji wa visima,
ujenzi wa josho, uchimbaji wa lambo na utengenezaji wa majiko banifu. Wengine
katika picha, wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Josephat Maganga
na Meneja wa Ruwasa Mhandisi Cyprian Warioba.
Uongozi wa Wilaya ya Mpwapwa umepewa siku Arobaini na tano kukamilisha usimikaji wa mabomba na matanki ya kuhifadhi maji safi na salama kwenye vijiji vya Mbugani, Ngh’ambi na Kiegea katika Wilaya ya Mpwapwa.
Agizo hilo limetolewa leo Desemba
23, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua Utekelezaji wa
Mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini ulipo chini ya Ofisi
ya Makamu wa Rais na unatekelezwa katika Wilaya tano nchini ambazo ni Mpwapwa,
Mvomero, Kishapu, Simanjiro na Kaskazini – A
Akiwa Wilayani Mpwapwa katika kijiji
cha Nghambi Dkt. Jafo amekasirishwa na kitendo cha mkandarasi wa Kampuni ya Make
Engineering kutoka Dar es Salaam kutokamilisha kwa wakati
mradi wa uchimbaji wa visima vyenye urefu wa mita 150 na kumuagiza mkandarasi
huyo kukamilisha kazi mapema iwezekanavyo.
Amesema azma ya Serikali ni
kuhakikisha huduma zinasogezwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
"Natoa siku Arobaini na tano tu maji yaanze kutoka hapa, mradi huu
ukamilike. Wananchi hawa wanataka maji mapema, hakuna kwenda sikukuu na
watumishi acheni kukaa maofisini, simamieni hili kikamilifu" Alisisitiza
Dkt. Jafo.
Aidha, ametoa rai kwa wakazi wa Mbugani,
Ngh’ambi na Kiegea kutumia vizuri mvua zinazonyesha kwa kupanda miti kwa vingi
ili kulinda mazingira, na kusisitiza kuwa agenda ya mazingira ndio kipaumbe cha
Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw.
Josephat Maganga amesema atahakisha ndani ya siku arobaini na tano kazi zote
zinakamilika na huduma ya maji inatolewa kwa wananchi.
Mradi wa kuhimili badiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini unafadhiliwa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Nchi Maskini kupitia Mfuko wa Dunia wa Mazingira ambapo kuna shughuli za uchimbaji wa visima, ujenzi wa josho, uchimbaji wa lambo na utengenezaji wa majiko banifu. Miradi yenye jumla ya Tshs. 2,257,042,400/- imeidhinishwa kutekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa.
No comments:
Post a Comment