Habari za Punde

TIA: Endelea Kupambana na Mabadiliko ya Teknolojia.

Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Leonard Mkude akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa mahafali ya 19 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyohusisha Kampasi ya Dar es Salaam na Mtwara yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Na Josephine Majura na Tusa Mwambenja, WFM, Dar es Salaam

SERIKALI imeipongeza Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), kwa kutoa mafunzo yanayowaandaa wahitimu kukidhi mahitaji ya soko kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda na ukuaji wa Teknolojia.

 

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Leonard Mkude, wakati wa mahafali ya 19 ya Taasisi hiyo yaliyohusisha wahitimu kutoka Kampasi ya Dar es Salaam na Mtwara yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Bw. Mkude alisema wahitimu wakijengewa uwezo vizuri watakua kwenye nafasi nzuri ya kushindana katika soko la ajira duniani lakini pia wataweza kujiari.

 

“Nawapongeza kwa kuendelea kuwajengea uwezo wananchi wa sekta mbalimbali kupitia mafunzo na huduma za ushauri zinazotolewa na Taasisi yenu”alisema Bw. Mkude.

 

Aliitaka Taasisi hiyo kuendelea kubuni mbinu zaidi katika utoaji huduma za utafiti na ushauri kwa kuwa zina mchango mkubwa katika kuzalisha mapato ya nchi.

 

Bw. Mkude alisema kuwa ufanyaji wa tafiti huisaidia Serikali kupata majawabu ya changamoto mbalimbali ambazo Taifa linakabiliana nazo katika jitihada za kuimarisha uchumi.

 

Aliitaka TIA, kuendelea kujitangaza ili kuweza kuwafikia wananchi wa kawaida hususan waliopo kwenye maeneo ya pembezoni ili watambue na kunufaika na fursa za mafunzo, utafiti na ushauri mbalimbali zinazotolewa na Taasisi hiyo.


Aidha alitoa wito kwa wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kama chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira.

 

Bw. Mkude aliwaasa wahitimu hao kwamba wakienda makazini wahakikishe wanafanya kazi kwa bidii, uadilifu, ubunifu, umakini, weledi na kujiepusha na uzembe kwa kuzingatia Sera, Sheria, Taratibu na Kanuni mahali pakazi.

 

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Taasisi ya Uhasibu Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu nchini zinazotoa mafunzo kwa viwango vya Kimataifa.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Taasisi hiyo Wakili Said Musendo Chiguma, alisema kuwa wahitimu wa TIA wamekuwa na utendaji kazi uliotukuka katika Sekta za Umma na Binafsi kutokana na mrejesho wanaoupata kupitia waajiri mbalimbali nchini.

 

Aliongeza kuwa hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi mwaka hadi mwaka licha ya kuwepo vyuo vingi vya ushindani ambapo Taasisi inajumla ya wanafunzi 25,249 ikiwa ni ongezeko la asilimia 71 kutoka wanafunzi 14,800 waliodahiliwa mwaka 2016.

 

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Dkt. Momole Kasambala alisema kuwa wameendelea kuboresha mitaala ya elimu ili iendeane na soko la ajira na kuwawezesha wahitimu kujiajiri.

 

Dkt. Kasambala aliongeza kuwa TIA imefanikiwa kuanzisha Kozi za Shahada ya Uzamili zipatazo 5, ikiwemo Shahada ya Sayansi katika Uhasibu na Fedha, katika Ugavi na Ununuzi, Ubunifu katika Usimamizi wa Miradi, Uongozi na Rasilimali Watu na Tehama pamoja na Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Masoko na Uhusiano wa Umma.

 

Aliongeza kuwa TIA imefanikiwa kuanzisha ushirikiano na vyuo nane vya nje ya nchi vikiwemo Vyuo Vikuu vya India, Ukraine na Kenya ambapo hatua hiyo itawezesha Wahadhiri na Wanachuo kuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu ili kuleta tija kupitia ushirikiano huo.

 

Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Uhasibu yamejumuisha wahitimu 7,131 kutoka Kampasi ya Dar es Salaam na Mtwara yenye jumla Wanawake 3,677 sawa na asilimia 51.6 ya wahitimu wote, na Wanaume 3,454 sawa na asilimia 48.4 ya wahitimu wote, wahitimu hao wametunukiwa Cheti cha Awali, Astashahada, Stashahada, Shahada na Stashahada ya Uzamili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.