Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Mhe. Selemani Jafo akifungua mkutano wa wadau mbalimbali wa mazingira wa kutoka Dodoma uliofanyika leo Januari 26, 2022 jijini hapa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo leo Januari 26, 2022 amekutana na wadau wa Mazingira wa Jiji la Dodoma kutoka sekta binafsi na taasisi za Serikali kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja katika kuendelea kutekeleza kwa vitendo kampeni ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
Amesema ili kuwa na Kampeni
endelevu ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa wadau katika ngazi zote na
kusisitiza kuwa kila mmoja aweze kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha Dodoma
inakuwa ya kijani na kutoa rai kwa jamii kutumia mvua zinazoendelea kunyesha
kupanda miti kwa wingi.
“Zoezi la kukijanisha Dodoma linaendelea kwa kupanda
miti maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma ambapo zaidi ya miti 40,000
imeshapandwa katika maeneo ya viwanja vya Chuo kikuu cha Dodoma, Mji wa
Serikali Mtumba, Eneo la Medeli na maeneo ya kuzunguka Shule za Msingi na
Sekondari zilizopo Dodoma” Dkt. Jafo alisisitiza
Pia ametoa wito kwa jamii kufuata taratibu na kuzingatia Sheria na kuacha
kujishughulisha na shughuli zisizoendelevu ikiwemo uchomaji wa moto hovyo
katika maeneo mbalimbali, hususan maeneo ambayo miti inapandwa
Nae Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Bw. Edward Nyamanga ametoa wito kwa sekta
binafsi na Wafanyabiashara wa aina mbalimbali Jijini Dodoma kushiriki kwa dhati
katika kuunga mkono serikali kwenye azma yake ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani
na kuwa Jiji la mfano nchini katika masuala ya Hifadhi na Usafi wa mazingira.
Lengo la kuanzishwa Mpango wa kupanda miti wa
kukijanisha Jiji la Dodoma ni kuhakikisha kuwa maeneo ya wazi, pembezoni mwa
barabara, makazi pamoja na maeneo ya kuzunguka mashamba yanapandwa miti ili
kuhifadhi mazingira na kupendezesha jiji la Dodoma. Kila eneo inapendekezwa
kupandwa aina ya miti inayofaa kulingana na sehemu husika
Kwa upande wake Meya wa Jiji
la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe amesema zoezi la upandaji miti liwe endelevu
na kutoa rai kwa Serikali kuepuka zoezi la upandaji miti wakati wa maadhimisho
na sherehe za kitaifa pekee.
Jumla ya wadau 70
wameshiriki katika kikao hicho kilichofanyika katika Hotel ya Morena, Dodoma na
kuhusisha wadau wa mazingira wa Jiji la Dodoma kutoka sekta binafsi na taasisi
za Serikali.
No comments:
Post a Comment