Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo alipozungumza na Mabalozi walioteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika Nchi mbali mbali walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa kuagana nao na kupata maagizo katika utekelezaji wa kazi zao .[Picha na Ikulu] 05/01/2022.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisisitiza jambo alipozungumza na Mabalozi walioteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika Nchi mbali mbali walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa kuagana nao na kupata maagizo katika utekelezaji wa kazi zao .[Picha na Ikulu] 05/01/2022.
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
05.01.2022
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza haja kwa Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya nchi walioteuliwa hivi karibuni kuipa kipaumbele Sera ya Diplomasia ya Uchumi katika nchi wanazokwenda kufanya kazi.
Rais Dk. Mwinyi alieleza hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walioteuliwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Miongoni mwa Mabalozi hao ni Balozi Perera Ame Silima anaekwenda Jamhuri ya visiwa vya Comoro, Balozi Said Shaib Mussa, anaekwenda nchini Kuwait, Balozi Fredrick Ibrahim Kibuta anaekwenda nchini Urusi, Balozi Profesa Adelardus Kilangi anaekwenda nchini Brazil, Balozi Alex Gabriel Kalua anaekwenda nchini Israel na Balozi Said Juma Mshana anaekwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao kwamba Sera ya Diplomasia ya Uchumi ndiyo iliyopewa kipaumbe hivi sasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo, ni vyema Mabalozi hao wakaenda kuifanyia kazi Sera hiyo ili uchumi wa Tanzania uzidi kuimarika.
Aliongeza kuwa kwa
upande wa Zanzibar sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta iliyopewa kipaumbele kupitia
uchumi huo wa Buluu na kuwasisitiza Mabalozi hao katika kuhakikisha wanaitumia
fursa hiyo kuitangaza Zanzibar kiutalii katika nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Dira ya Uchumi wa Buluu inaweza kufanya kazi kwa nchi zote wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania Mabalozi hao hivyo, alisisitiza haja ya kuwakaribisha wawekezaji kuja kuekeza katika maeneo kadhaa ya viwanda hapa nchini.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Miwnyi alisisitiza kwamba kwa upande wa nchi ya Comoro ni vyema hatua za kurejesha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara ukafufuliwa kati ya nchi hiyo na Zanzibar.
Nao Mabalozi hao kwa upande wao walimuhakikikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba maelekezo na nasaha alizowapa watazifanyia kazi na kueleza kuwa itakuwa ni Dira yao katika utekelezaji wa kazi zao wakiwa katika vituo vyao vya kazi nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mapema, Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ukiongozwa na Mwakilishi Mkaazi Christine Musisi.
Katika mazungumzo hayo UNDP imekubali kutuma timu ya Wataalamu ili kushirikiana na wataalamu waliopo Serikalini, ikiwa ni hatua ya kupata njia bora ya utekelezaji wa mipango ya Maendeleo kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo uchumi wa Buluu, kwa lengo la kupata mafanikio .
Aidha, wataalamu hao watapata fursa ya kupanga mikakati ya
maendeleo katika kipindi cha muda mfupi na muda mrefu kitaifa na Kimataifa,
sambamba na kufuatilia utekelezaji katika maeneo ya kipaumbele.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment