Habari za Punde

Mke wa Rais wa Zanzibar pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation Aongioza Mamia ya Wananchi na Vikundi vya Mazoezi Mkoa wa Kusini Unguja leo.

 

Mke wa Rais wa Zanzibar ambaeni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation Mama Mariam Mwinyi akiwasalimia Wananchi wa Muyuni akiwa katika matembezi ya mazoezi ya Viungo yaliofanyika katika Kijiji cha Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja leo na (kushoto kwake) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa mazoezi ni umoja, mshikamano, upendo na mwisho wa siku ni amani.

Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika uwanja wa mpira wa Muyuni, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kumaliza mazoezi aliyoyaongoza ambayo yalianzia Muyuni ‘C’, hadi Muyuni ‘B’, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusni Unguja.

Alisema kuwa mazoezi ni umoja, amani mshikamano, jambo ambalo limeonekana katika mazoezi hayo ambayo yamewashirikisha wananchi mbali mbali kutoka vyama vyote vya siasa.

Alisema kuwa matembezi hayo ni ahadi yake aliyoitoa mnamo Febuari 19 mwaka huu wakati akizindua taasisi yake ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF),ambapo aliahidi kuwa yeye atakuwa championi na kinara katika kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi.

Aidha, alisema kuwa ufanyaji wa mazoezi ni maendeleo kwani humfanya mtu kuwa mkakamavu na kuwa na akili ya kuweza kufanya kazi kwa uchangamfu  na ufanisi mkubwa.

Alisema kuwa ufanyaji wa mazoezi unasaidia kujikinga na maradhi yote yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, presha,uzito uliozidi kipimo ambayo yote hayo yanaweza kuzuiwa na ufanyaji wa mazoezi.

“Mimi kwangu ninachotaka tufanye  mazoezi kwa kutembea pamoja, ili tupate afya na mwisho wa siku tujenge amani”, alisisitiza Mama Mariam Mwinyi.

Mama Mariam Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), alisema kuwa mazoezi hayo yataendelea katika Wilaya na Mikoa mengine yote ya Unguja na Pemba.

Nae Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwitia, alimshukuru Mama Mariam Mwinyi kwa kuleta wazo hilo la kufanya mazoezi na kuahaidi kwamba Wizara yake inamshukuru kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

Aidha, Waziri Tabia alimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa kuitekeleza kwa vitendo Sera ya Michezo ya mwaka 2018 ambayo inasisitiza kuwahamasisha wananchi nchi nzima kufanya mazoezi na kutengeneza mazingira ya kuwashirikisha kushiriki katika michezo ili kuepukana na maradhi yasiyoambukiza.

Aliongeza kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo pamoja na viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wataendelea kumuunga mkono kupitia taasisi yake ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) kutokana na juhudi zake kubwa anazozichukua za kuwaunganisha wananchi.

Nao viongozi wa Mkoa wa Kusini walitoa shukurani kwa Mama Mariam Mwinyi kwa kuanza jambo lake hilo la mazoezi katika Mkoa na Wilaya ya Kusini na kueleza jinsi walivyofarajika.

Viongozi mbali mbali walishiriki katika mazoezi hayo wakiwemo wake wa viongozi wakuu wa kitaifa hapa Zanzibar akiwemo Mke wa Makamo wa Kwanza wa Rais Mama Zainab Kombo Shaib, Mke wa Makamo wa Pili wa Rais, Mama Sharifa Omar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mama Shamsi Vuai Nahodha pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa na  serikali, wananchi pamoja na vikundi mbali mbali vya mazoezi.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.