Habari za Punde

GCLA yawapiga msasa Wanasheria

Na Fatma Salum- GCLA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetoa elimu kwa Wanasheria na Mawakili ambao pia ni wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) mkoani Arusha kuhusu majukumu na  sheria mbalimbali zinazosimamiwa na Mamlaka hiyo ili kuendelea kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria hizo.

Akizungumza katika mafunzo hayo Meneja wa Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba, Hadija Mwema alisema kuwa lengo la GCLA ni kuwawezesha wanasheria kupata uelewa zaidi kuhusu utekelezaji wa sheria za Mamlaka, utaratibu na kanuni za uchukuaji wa sampuli za sayansi jinai na vinasaba hivyo kurahisisha majukumu yao wanapokuwa mahakamani.

“Tunaamini elimu hii tunayoitoa kwa wanasheria itawasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa wao ni miongoni mwa wanaotambulika kama mamlaka inayoweza kuomba kipimo cha vinasaba (requesting authority) kwa mujibu wa sheria,” alieleza Hadija.

Akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya GCLA, Meneja wa Maabara ya Maikrobaiolojia, John Wanjala alisema kuwa wanasheria ni wadau wakubwa wa mamlaka hiyo kwa sababu wataalamu wake hutoa ushahidi wa kitaalamu kwenye mashauri mbalimbali mahakamani ili kusaidia kupatikana kwa haki katika jamii.

Naye Mwanasheria wa GCLA, Abeid Kafunda aliwaeleza mawakili hao kuwa majukumu yote ya Mamlaka hiyo hutekelezwa chini ya sheria tatu ambazo ni Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Namba 8 ya mwaka 2016, Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba 3 ya mwaka 2003 na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Vinasaba vya Binadamu Namba 8 ya mwaka 2009.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TLS mkoani Arusha, Wakili George Njooka aliishukuru GCLA kwa elimu waliyopatiwa na kuiomba Mamlaka ikatoe elimu hiyo vyuoni kwa wanafunzi wanaosomea sheria hususan Shule ya Sheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania) kwa sababu utekelezaji wa sheria hizo sio sehemu ya mafunzo wanapokuwa vyuoni.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeweka utaratibu wa kutoa elimu kwa umma na mafunzo mbalimbali kwa wadau kuhusu majukumu yake ili kurahisisha utekelezaji wa kazi zake na kusaidia jamii kwa ujumla. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.