Habari za Punde

DARASA LA CHANETA

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Mei 20, 2022 niliingia Bungeni nikiambatana na viongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao waliwapokea viongozi wa CHANETA-Chama Cha Mpira wa Netiboli Nchini waliokuwa wageni wa Naibu Waziri Pauline Gekul.

Mara zote ninapokuwa na mtu mgeni lazima kuna jambo huwa najifunza kwake, je CHANETA walinipa darasa la nini?

Darasa lao lilikuwa la Mchezo wa Netiboli tu ambalo lilijikita katika masomo makubwa mawili. Kwa kuwa mimi ni mkarimu ngoja nikugawie masomo hayo.

Somo la kwanza lilikuwa juu ya jina halisi la mchezo wa NETIBOLI, niliambiwa kuwa jina lao na siyo mpira wa pete kama linavyotumika na baadhi ya wadau bali mchezo wa NETIBOLI.

“Mchezo wetu ni kweli unayo hiyo pete, una nyavu, unao mlingoni. Pete inayotajwa ina kipenyo cha milimita kati ya 380-450, mlingoni unakuwa na urefu wa mita 3.55 ambapo nusu mita huwa inazama ardhini wakati inachimbiwa na mlingoni ukiwa uwanjani una urefu wa mita 3.05.”

Haya aliniuma sikio Dkt Devotha Marwa ambaye ndiye mwenyekiti wa CHANETA.

Kiongozi huyo wa chama cha michezo huu nchini alisema kuwa urefu wa uwanja wa mpira wa netiboli ni mita 30.50 na upana wake ni mita 15.25 ndiyo kusema Mita 30.50 kwa Mita 15.25. Unaposema mpira wa pete ni kuviweka kando vifaa vyote vinavyotumika kuukamilisha mchezo huo kuchezwa.

“Uwanja wa Netiboli unatazama kati ya Kaskazini na Kusini ili kutoa nafasi ya jua linapochomoza na kuzama kutoelemea wachezaji wa upande mmoja. Kila timu inaonja joto ya jiwe la jua uwanjani. Kama uwanja huo ungekuwa unatazama Mashariki na Magharibi hali hiyo ingependelea timu moja na kuumiza timu nyingine kwa miale ya jua.”

Dkt.Marwa alidai kama uwanja wa Netiboli ukiwekwa vizuri unaweza kutumiwa hata kwa michezo mingine kama vile mpira wa wavu kwa kuwa vipimo vyake havitafautiani sana.

“Tunawahimiza Watanzania wengi kuupenda na kuucheza mchezo huo kwani kiwanja kinaweza kuchezwa hata kikiwa na majani, mchanga na sakafu. Gharama za vifaa vyote tangu pete, mlingoni, mpira, wavu na kuweka sawa uwanja ni shilingi 200,000/ Je kwanini watoto wetu hawachezi mchezo huo?” Aliuliza.

Hayo yote yalitoka katika somo la kwanza la CHANETA.

Somo la pili lilijikita katika vionjo vya ndimi zangu zilipowatazama viongozi hawa, walikuwa ni watu wa mazoezi kweli kweli huku wakiwa na siha zilizojengeka vizuri sana. Katika michezo mambo yanapendeza mno kama viongozi wa vyama vya michezo waliwahi kuucheza mchezo huo, mathalani TFF na BMT enzi za Leodga Tenga katika soka.

Dada zangu watatu Shy-Rose Bhanji, Beth Mkwasa na binti mmoja ambaye jina lake japokuwa nililihusudu kulijua lakini sikujaliwa kulipata, wao walikuwa na miili ya wastani huku ikiwa imara sana, nikasema kweli Netiboli imepata uongozi.

Nilipouliza juu ya wao kuucheza mchezo huo nilijibiwa kuwa wote ni mabingwa wa kuucheza na kuufundisha mchezo huo. Shy-Rose Bhanji niliambiwa anacheza CENTER(C) Beth Mkwasa GOAL KEEPER (GK) naye Dkt. Devotha Marwa WING DEFENCE (WD) binti niliyetamani kulifahamu jina lake lakini wapi yeye niliambiwa anacheza GOAL SHOOTER (GS) hizo zote habari ndogo, habari kubwa ipo kwa WINGER ATTACK (WA)-Rose Mkisi, GOAL DEFENCE (DF)–Hilder Mwakatobe na GOAL ATTACK (GA)-Mary Chalamila.

Narudi kulisema kwa Rose Mkisi na Mary Chalamila maana habari zao zilikuwa makini  mno katika kuucheza mchezo huo. Kweli Netiboli kumekucha, lakini nisiumalize uhondo huo.

Wakiwa uwanjani watajipanga hivi GK-GS,WA-WD,GA-GD,C-C,GA-GD,WD-WA na GS-GK. Ndiyo kusema Mkwasa, Mkisi, Chalamila, Bhanji, Dkt Marwa, na yule binti nisiyemfahamu jina atacheza–Goal Shooter. Huku Shukuru Kiwege na Kilongozi Ray wakiisimamia timu hiyo.

Kwa maelezo ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul ni kuwa timu bora za Netiboli zipo nyingi sana hasa hasa timu ya TAMISEMI. Kwa kauli hiyo ya natamani uongozi wa CHANETA ucheze mechi ya kirafiki na timu ya TAMISEMI.

Mie mwanakwetu nitakuwa kando kuukodolea macho mpambano huo, naisubiri siku hiyo kwa hamu kubwa. Nyie si mnapenda soka? Endeleeni na habari za Simba na Yanga za kupandishana  presha mie naendele na Netiboli yangu,

Huku timu zetu zinachanja mbuga kimataifa kila uchao.

Kabla ya mpambano huo kufanyika naomba nitoe rai kwa timu ya Netiboli ya TAMISEMI chonde chonde msiniumizie Dkt Devotha Marwa katika mechi hiyo.

Hadi hapo masomo yangu mawili ya darasa la CHANETA yamekwisha.

Maswali yanakaribishwa

makwadeladius@gmai.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.