Habari za Punde

Dk.Mwinyi Ameupongeza Utayari wa Uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha Nchini Norway Kujenga Hospitali ya Kisasa ya Maradhi ya Moyo Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Wafadhili kutoka Uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha Nchini Norway ukiongozwa na Mfadhili Bw.Trond Mohn (kulia kwa Rais)  wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 15-6-2022, kuelezea ufadhili wao wa Ujenzi wa Kituo cha Matibabu ya Moyo Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Wafadhili kutoka Uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha Nchini Norway ukiongozwa na Mfadhili Bw.Trond Mohn (kulia kwa Rais)  wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 15-6-2022, kuelezea ufadhili wao wa Ujenzi wa Kituo cha Matibabu ya Moyo Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Kiongozi wa Ujumbe wa Wafadhili kutoka Chuo Kikuu cha Hauklend kutoka Nchini Norway Bw.Trond Mohn, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 15-6-2022

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha nchini Norway kujenga Hospitali ya kisasa ya maradhi ya moyo hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha nchini Norway ambao ulimuhakikishia Rais Dk. Miwnyi kwamba uko tayari kuanza ujenzi huo hivi karibuni.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ujenzi wa Hospitali hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma za maradhi ya moyo hapa Zanzibar na kupunguza kuwasafirisha nje ya nchi wagonjwa wenye maradhi hayo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano kati yake na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukland ambao ulianzishwa tokea mwaka 2007 ambao umeweza kuzaa matunda na iko tayari kuuendeleza.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya Hospitali kwa ajili ya akina mama na watoto katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, kusaidia ujenzi na vifaa katika hospitali ya Kidongo chekundu pamoja na kusaidia vifaa tiba kadhaa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha na kuendeleza miradi mbali mbali katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuendeleza mafunzo kwa wauguzi na madaktari wazalendo sanjari na kubadilishana uzoefu.

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuimarisha mifumo katika sekta ya afya hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Nao uongozi wa Wizara ya Afya ulieleza mahusiano na mashirikiano yaliopo kati ya Hospitali hiyo na Hospitali ya Mnazi Mmoja huku uongozi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja ukieleza mafanikio makubwa yatakayopatikana baada ya kukamilika na kuanza kazi kwa Hospitali hiyo kutokana na maradhi ya moyo kuwa ni maradhi yalioshika kasi hapa nchini na duniani kwa jumla.

Nao uongozi huo wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha nchini Norway ulimueleza Rais Dk. Mwinyi azma yao ya kujenga Hospitali kwa ajili ya kutoa huduma za maradhi ya moyo hapa Zanzibar.

Katika maelezo yao uongozi huo ulimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba wako tayari kuanza ujenzi huo ndani ya mwaka huu kwani wameshajipanga kuanza ujenzi wa mradi huo mkubwa.

Pamoja na hayo, uongozi huo ulisisitiza kwamba hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi zao wanazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha wanaendeleza uhusiano na ushirikano uliopo ambao umeanzishwa maalum kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar. OF RESPONSIBILITY

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.