Habari za Punde

TUPENDE NYUMBANI KWETU

 
Na.Adeladius Makwega-BUJORA MWANZA.

Wakati Tamasha la Utamaduni la Bulabo likiingia siku yake ya tatu katika eneo la Bujora wilayani Magu mkoani Mwanza huku burudani za ngoma za kabila hili zikilisindikiza tamasha hilo mithili ya maji yanayotiririka mtoni wakati wa masika, Leo hii mwanakwetu naomba nimtazame kiongozi wa dini aliyenivutia na kiongozi pekee wa dini aliyeshiriki Tamasha la Bulabo.

Wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo Mhashamu Baba Askofu Mkuu, Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza alishiriki tangu mwanzo hadi mwisho. Kwa faida ya msomaji wangu tambua kuwa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza lilianzishwa mwaka 1880 hilo ni miongoni mwa majimbo ya zamani hapa nchini.

Huku Baba Askofu Nkwambe akiwa ni askofu wa tisa mpaka sasa, akipokea kutoka kwa  Baba Askofu Yuda Ruwa’ichi ambaye sasa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Askofu wa Kwanza wa Jimbo hilo alikuwa ni Baba Askofu Jean–Joseph Hirth.

“Tamasha hili huwa linafanyika kila mwaka na lilianzia kule Sumve jirani na Kanisa la AIC na hatimaye hapa Bujora, kwa sasa linafanyika kwa mwaka wa 82. Kwetu sisi Wasukuma ni heshima kubwa kwa kuwa tamasha la Bulabo linatupatia furaha kubwa mno.”

Haya ni maneno yake ya utangulizi ambayo yaliwezwa kunasa na mashine yangu ya kurekodi sauti akiwa amesimama akitoa neno la shukurani kwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Bulabo jioni ya Juni 19, 2022.

Tangu siku ya asubuhi ya ufunguzi nilibaini kuwa Kanisa katoliki Jimbo kuu la Mwanza tangu enzi waliweka uwekezaji mkubwa katika utamaduni wa Wasukuma kwa kujenga Makumbusho ya Bulabo.

Ndiyo kwanza waliwekeza muda wa kufanya utafiti na kukusanya zana na vitu kadhaa vya utamaduni huo, alafu wakawekeza fedha kukamilisha kilichokusanywa na kukihifadhi makumbusho hayo-Hayo nimeyabaini hapa hapa katika Tamasha la Bulabo.

Nilipomtazama Baba Askofu Nkwambe nilibaini kuwa ni mtu mmoja mnyenyekevu, mkarimu, mpenda watu, anayejishusha na anaheshimu mamlaka zingine si serikali tu bali hata Watemi wa Kisukuma.

“Tukipata barabara inayotufikisha katika makumbusho yetu litakuwa ni jambo kubwa sana, pia tukipata vibali vya nyara na nyaraka tulizo nazo na tunazotumia zile za asili  hasa kwa viongozi wa jadi itakuwa ni heshima kubwa sana.”

Akiwa amevalia kanzu yake nyeupe yenye vifungo vya rangi ya dhambarau, Baba Askofu Mkuu Nkwambe alisema maneno hayo.

Akitamka maneno ya kiswahili taratibu huku akiziunganisha konsonati na irabu kwa ufasaha mkubwa aliwaambia wananchi walioshiriki ufunguzi huo kuwa yeye anaamini kimaendeleo Wasukuma wapo mahali pazuri, lakini wakiweka bidii zaidi watafika mbali zaidi, kwa juhudi za pamoja za wananchi na viongozi wao.

Macho yangu yalishuhudia hilo katika sekta ya elimu, shule nyingi katika ukanda huo zina mandhari nzuri sana huku zikiwa zimepigwa rangi inayofanana kwa madarasa yote kwa shule nzima. Mandhari hiyo ni adimu sana kwani maeneo mengi shule zetu unakutana na mandhari ya madarasa mawili mazuri mengine hali zake inasikitisha.

“Watemi waliunganisha sana watu, Wasukuma ni kabila kubwa na tumeenea sehemu mbalimbali, watemi hawa walituunganisha, walifanya tujisikie tu kitu kimoja na ni mara chache sana huku Usukumani uliweza kusikia vita, hii ni kwa sababu ya hawa hawa watemi na hata sasa ni mara chache unaweza kusikia kuna ubaguzi kuwa huyu ni Msukuma wa mashariki na huyu wa magharibi, sisi kwa kweli ni kitu kimoja.”

Alisisitiza haya huku wananchi waliojitokeza wakiwa kimya wakimsikiliza kiongozi huyu wa dini, sikushuhudia mtu yoyote aliyesimama japokuwa Baba Askofu alizungumza wa mwisho.

“Yote haya ni mafanikio ya viongozi wetu wa jadi, ningeomba muendelee kuilea hivyo hivyo jamii ya Wasukuma na watu wote wa maeneo haya na kwa kufanya hivyo watajisikia wapo kitu kimoja na Watanzania wengine.” Alisisitiza.

Akmalizia salaam zake za shukurani alisema kuwa kuna siku moja alikuwa nje ya nchi  alikutana wa mzungu ambaye alikuwa akisoma na waafrika wengi. Ulipofika wakati wa likizo waafrika wengine waliamua kwenda likizo Ulaya na Marekani lakini Watanzania wote walirudi nyumbani Tanzania.

“Jambo hilo lilimshangaza sana ndugu huyo na akasema nyinyi Watanzania mnapenda sana nyumbani kwenu. Kwa hiyo ndugu zangu tupende nyumbani kwetu na kwa kufanya hivyo tutapendana sisi kwa sisi na tutapenda vyote vilivyo vyetu kama vile utamaduni wetu.”

Alipoitimisha  maneno haya Baba Askofu Mkuu Nkwambe, shughuli ya ufunguzi ilikamilika  lakini burudani ziliendelea kurindima hadi usiku wa siku hiyo.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.