Habari za Punde

Wadau Waipongeza Taasisi ya "Mwanamke Initiatives Foundation " MIF Kwa Kusaidia Mtoto wa Kike Zanzibar Wliojitokeza Kuchangia.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation Mhe. Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge na mtetezi wa haki  za Vijana na Wanawake amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza ambapo amewaomba kuendelea  kuchangia ili kuwasaidia Watoto wa kike  waweze kutimiza ndoto zao.

Na John Mapepele. 

Wadau mbalimbali wa kupigania maendeleo ya mtoto wa kike nchini wamejitokeza  kuchangia takribani  shilingi  bilioni moja  kwenye  taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) iliyopo Zanzibar inayojishughulisha na kumkwamua mtoto wa kike katika elimu ili kutimiza ndoto zake. 

 Wadau hao wametoa michango  hiyo katika  halfa maalum ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na taasisi ya (MIF) usiku wa kuamkia leo Juni 19, 2022 Zanzibar  kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na mfuko huo  katika suala zima la  kuwasaidia Watoto wa kike kufikia malengo  yao hivyo kuendesha maisha yao.

Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mfuko huo, Mhe. Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na mtetezi wa haki  za vijana na wanawake amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza ambapo amewaomba kuendelea  kuchangia ili kuwasaidia Watoto wa kike  waweze kutimiza ndoto zao.

“Naomba kuchukua  fursa hii kushukuru sana isiwe mwanzo wala mwisho naomba iwe mwanzo na tuendelee kuchangia  mfuko wetu wa Mwanamke Initiative ili kuona kwamba mtoto wa kike anasimama  na anaweza kushindana katika ulimwengu” amefafanua,  Mhe Wanu.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti tofauti kuhusu kuanzishwa kwa mfuko huo, wamepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na MIF kwa kuwasaidia watoto wa kike Zanzibar huku wakitoa rai kwa wadau wengi zaidi  kushiriki kwenye jitihada hizo za kuwakomboa Watoto wa kike kwa kuchangia kwa hali na mali katika mfuko huo ili lengo liweze kutimia. 

“Tumefarijika sana na kazi kubwa na nzuri zinazofanywa na mfuko huu, tunaomba na wadau wengine waendelee kujitokeza kuchangia kwa  kuwa ukimsaidia mtoto wa kike aweze kujikwamua umesaidia taifa”aliongeza Tuli Mwambapa ambaye ni Mkurugenzi wa Benki ya CRDB nchini.

Benki ya CRDB imechangia shilingi milioni mia tatu ambapo wadau wengine pia waliweza kuchangia kwenye hafla hiyo.

Katika hafla hiyo mbali na wageni mbalimbali waliohudhuria   pia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa ambaye ni mume wa Wanu alishiriki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan. leo,  Juni 19, 2022 anatarajiwa kuuzindua rasmi mfuko huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.