Habari za Punde

Kikao cha Saba cha Sensa Tanzania Ukumbi wa Mikutano wa Kumataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam




Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipowasili katika Ukumbi wa Julius Nyerere Convention Center Jijini Dar-es-salaam kuongoza Kikao cha Saba cha Kamati hiyo.
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ambae ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiakhirisha Kikao cha Saba cha Kamati hiyo kilichofanyika Ukumbi wa Julius Nyerere Convention Center Jijini Dar-es-salaam kilichoketi chini ya Mwenyekiti wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya wa Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambae ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiongoza Kikao cha Saba cha Kamati hiyo kilichofanyika Ukumbi wa Julius Nyerere Convention Center Jijini Dar-es-salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipokea moja ya Kishkwambi kutoka kwa Balozi wa Korea ya Kusini Nchini Tanzania Mhe. Kim Sun Pyo ikiwa ni Mchango wa Korea ya Kusini kuchangia Vishkwambi Mia sita (600)katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Nchini Agosti 23 Mwaka huu.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka Wajumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi kuendelea kufatilia kwa karibu Maandalizi ya Sensa ya Mwaka huu ili kukamilisha kwa ufanisi wa Zoezi hilo.

Mhe. Majaliwa ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi ameeleza hayo katika Kikao cha Saba cha Kamati hiyo kilichofanyika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre  Jijini Dar-es-Salaam.

Amesema hadi sasa Matayarisho ya Sensa ya Mwaka huu yamefikia Asilimia Tisini na Sita (96)  iliyotokana na  mashirikiano ya Wajumbe wa Kamati hiyo ambapo amewashukuru Wajumbe hao kwa hatua hiyo ambapo inaashiria kukamilisha kwa ufanisi zoezi hilo kwa mwaka huu.

Amesema kuelekea Siku ya Sensa Kitaifa Agosti 23 ni Wajibu wa Wajumbe hao kufuatilia kwa karibu Maafisa wa Sensa waliyopo katika Jamii ambao wanaendelea na Matayarisho ya Zoezi hilo ambapo kushirikiana nao kutawawepesishia Maafisa hao katika Majukumu yao.

Aidha Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa Siku ya kuanza kwa Zoezi la Sensa Agosti 23 iwe ni Siku ya Mapumziko ili kutoa Fursa kwa Wananchi kushirkiana na Makarani watakapofika katika makazi yao.

Aidha Mwenyekiti huyo amewashukuru Wananchi kwa kuunga Mkono Uhamasishaji wa Zoezi hilo hatua ambayo imeisaidia Wananchi wengi kuwa na uelewa wa Ushiriki katika Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na Viongozi wengine mbali mbali kuwa karibu na Makarani ili kuwasaidia wanapohitaji Msaada na kutatua changamoto wanakazokabiliana nazo.

Aidha Mhe. Hemed ambae ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wajumbe hao kuendelea kushirikiana ili kufanikisha kukamilika kwa zoezi hilo kwa ufanisi zaidi.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameendelea kuwataka Wananchi kutoa Taarifa sahihi watakapofikiwa na Makarani wanapokusanya Taarifa zao ili kufanikisha zoezi hilo na kuwatoa hofu wananchi kuwa Sensa hiyo haitoulizwa masuala binafsi

Nae Waziri Afisi ya Waziri Mkuu Mhe. George Simbachawene ameeleza kuwa Matayarisho ya Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi limefikia Asilimia Tisini na Sita (96) ambapo amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa  kipindi cha kuelekea Agosti 23 wataendelea kuwajibika ili kakamilisha Zoezi hilo kwa ufanisi zaidi.

Aidha amemueleza Mwenyekiti huyo kuwa Kamati hiyo itaendelea na Uwajibikaji hata baada ya Zoezi kukamilika ili kuhakikisha Taarifa zinakamilika kwa usahihi.

Awali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokea Vishkwambi Mia Sita (600) kutoka kwa Balozi wa Korea ya Kusini Nchini Tanzania Mhe. Kim Sun Pyo ambapo ameishukuru Serikali ya Korea ya Kusini kwa kutoa Msaada huo ambao utaongeza Idadi ya Vishkwambi vinavyohitajika katika kukamilisha Zoezi hilo.

Aidha Mhe. Majaliwa amepokea Fulana kutoka kwa Benki ya NMB   zenye gharama ya Shilingi Milioni Ishirini (20,000,000/=) kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo.

 Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

18/08/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.