Habari za Punde

Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari wa Kuwajengea Uwezo wa Masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza Walimu Unakwenda Sambamba na Mikakati ya Serikali ya Kuhakikisha Inatoa Elimu Bora.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Uzinduzi wa Muongozo wa Mafunzo ya Sayansi, Hesabati  na Kingereza kwa Skuli za Sekondari Zanzibar, uzinduzi huo uliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 3-8-2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari wa kuwajengea uwezo wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza walimu unakwenda sambamba na mikakati ya Serikali ya kuhakikisha inatoa elimu bora inayoendana na mahitaji ya sasa.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa mafunzo ya Walimu wa Sayansi, Hisabati na Kiingereza pamoja na makabidhiano ya Moduli na Miongozo ya Mafunzo, hafla iliyofanyika huko katika hoteli ya Golden Tulip, iliyopo uwanja wa ndege Zanzibar.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Elimu ya Sayansi na Hisabati ina mchango mkubwa katika kufikia malengo hayo.

Alisema kwamba ni dhahiri kuwa katika kufikia malengo hayo, ni lazima mikakati imara ya kuinua ufaulu wa masomo ya Sayansi na Hisabati sambamba na uwezo katika lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi uimarishwe.

Aliongeza kuwa katia kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2017 hadi 2021, matokeo ya wanafunzi katika mitihani ya Taifa ya kumaliza elimu ya Sekondari hayakuwa yakiridhisha.

Alisema kwamba kwa wastani asilimia 33 ya wanafunzi kila mwaka wanakosa vyeti na wengi wao ni wale wanaosoma masomo ya Sayansi ambapo ufaulu mdogo wa wanafunzi hasa katika masomo ya Sayansi na Hisabati unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa walimu wenye sifa, uhaba wa maabara na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa vitendo.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na washirika mbali mbali wa maendeleo ili kuhakikisha changamoto zinazoathiri ufaulu wa masomo ya Sayansi zinapatiwa ufumbuzi kwa kuwajengea walimu uwezo zaidi wa ufundishaji wa masomo hayo na pia, kujenga maabara za Sayansi na kuzipatia vifaa.

“Nafurahi kusikia kwamba tulianza kuwapatia mafunzo walimu 600 wanaosomesha Sekondari Kidato cha Kwanza na cha Pili kwa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kupitia Mradi wa ZISP ambao Serikali inautekeleza kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na leo tena kwa kushirikiana na KOICA tutawapatia mafunzo walimu wa Skuli za Sekondari wa Kidato cha Tatu na cha Nne wanaosomesha masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza Unguja na Pemba”,alisema Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Skuli zote mpya zinakuwa na maabara za Sayansi, maabara za Kompyuta na maktaba za kisasa pamoja na kuzipatia vifaa.

Alisema kuwa hayo ni miongoni mwa mageuzi makubwa ya Elimu ambayo Serikali inaendelea kuyafanyia kazi ambapo kupitia mageuzi hayo Serikali itaimarisha matumzi ya Teknolojia katika Skuli zote ili kurahisisha ufundishaji na kujifunza kwa walimu na wanafunzi hasa katika ngazi ya Elimu ya Msingi na Sekondari.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa matumizi ya Teknolojia yatawasaidia sana wanafunzi kuweza kujifunza popote walipo na si lazima kuwepo darasani kwani itakumbukwa wakati wa Janga la UVIKO-19, pale ambapo Skuli zilifungwa kwa takriban miezi mitatu na bado wanafunzi waliendelea kusoma.

Alisisitiza kwamba Serikali kupitia mageuzi ya Elimu itaimarisha mafunzo ya Amali na Ufundi kwa kuhakikisha kila Wilaya ina vyuo vya aina hiyo kwa ajili ya watoto ili waweze kupata ujuzi wa ufundi utakaowawezesha kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato kwa ajili ya kuimarisha maisha yao.

Rais Dk. Miwnyi alitoa wito kwa walimu wote wa Skuli za Serikali, waliengwa wa mafunzo hayo wanaofundisha masomo ya Hisabati, Sayansi na Kiingereza kushiriki kikamilifu katika kuyapokea mafunzo hayo na kwenda kuyafanyia kazi wakati wanapofundisha wanafunzi wao madarasani.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alilishukuru Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea washuku KOICA, ‘Good Neighbors’ na washirika wenzao wa maendeleo katika kutekeleza na kufanikisha miradi huo muhimu wa mafunzo ya walimu aliyayazindua. “Nawashukuru sana Serikali ya Korea ya Kusini, KOICA na Taasiasi ya Good Neighbors’ kwa msaada wao huo mkubwa katika sekta ya elimu”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Nae Wazir wa Elimu na Mafunzo ya Amali Leila Mohammed Mussa alitoa pongeza kwa KOICA kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katia kuimarisha sekta ya elimu.

Alieleza kwamba mbali ya msaada wao huo wa mafunzo kwa walimu wa Sayansi wa Sekondari pia, KOICA imesaidia katika ujenzi wa maabara  kumi za kisasa ya Sayansi Unguja na Pemba.

Alieleza juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu ambapo imetenga jumla ya TZS Bilioni 63 kwa ajili ya miradi ya elimu zinazotokana na fedha za ahuweni ya UVIKO-19.

Balozi wa Korea ya Kusini Sun Pyo Kim, kwa upande wake alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Korea ya Kusini itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake mbali mbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Balozi Kim alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake za kuiimarisha sekta ya elimu.

Mapema  Mkurugenzi Mkaazi wa KOICA Kyucheol Eo pamoja na Mkurugenzi Mkaazi wa ‘Good Neghbors’ kwa nyakati tofauti walieleza hatua wanazozichukua katika kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta ya elimu huku wakiahidi kuendeleza misaada yao ili kuhakikisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza mafunzo yake yanatolewa kwa ufanisi mkubwa.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikabidhiwa vitabu vya miongozo ya mafunzo na moduli  kwa walimu pamoja na Kamati za Skuli ambapo mapema mara baada ya kufika hoteli hapo alitembelea mabanda maalum yaliyowekwa nyenzo za kufundishia na kupata maelezo juu ya namna za kufundishia.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.