Habari za Punde

Ujerumani Kuipiga Jeki Tanzania Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi

Na.Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwingulu Lameck Nchemba, ameishukuru Ujerumani kwa kuahidi kuendelea kuisadia Tanzania kutekeleza Miradi yake mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vya ufundi (VETA) vitakavyosaidia kukabiliana na tatizo la ajira hususan kwa vijana nchini.

Mhe. Dkt. Nchemba ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, kutoka Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mhe. Dkt. Barbel Kofler, jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa kipaumbele cha Serikali ni kujenga vyuo hivyo vya ufundi katika Wilaya 72 ambazo hazina kabisa vyuo hivyo ili kutekeleza dira ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutatua changamoto ya ajira inayowakabili wananchi wake na kuiomba Ujerumani kusaidia ujenzi wa miundombinu ya vyuo hivyo pamoja na zana za kufundishia na kujifunzia.

“Eneo ambalo tumelizungumzia linaenda sambamba na mwelekezo wa Mhe. Rais Samia Sulu Hassan ni ujenzi wa Vyuo vya Ufundi (Veta) katika maeneo ya Wilaya ambazo hazina Vyuo vya Ufundi ili kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alimshukuru mgeni wake, kwa utayari wa Serikali yake wa kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuiuchumi na kijamii ambayo nchi hiyo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta za afya, elimu, hifadhi ya mazingira, utalii, afya na mingine mingi.

Kuhusu masuala mengine ya usawa wa kijinsia na udhibiti wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, Mheshimiwa Dkt. Nchemba, alimhakikishia Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, kutoka Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mhe. Dkt. Barbel Kofler, kwamba Serikali imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na masuala hayo.

Alisema kuwa uwakilishi wa wanawake katika vyombo ya maamuzi umeongezeka na hatua madhubuti zinachukuliwa kukabiliana na vitengo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, ameipongeza Ujerumani, kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kuwa hivi karibuni nchi hizo mbili zilitiliana saini mikataba mitatu yenye thamani ya Euro milioni 45 sawa na takribani shilingi za Tanzania bilioni 119.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu katika sekta za maji, afya na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.

“Tanzania imenufaika na misaada kutoka Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya maji, nishati, matumizi endelevu ya maliasili na utunzaji wa mazingira pamoja na usimamizi bora wa fedha za umma”, alisema Bw. Tutuba.

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, kutoka Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mhe. Dkt. Barbel Kofler, ameipongeza Serikali kwa jitihada mbalimbali wanazozifanya za kukuza uchumi, kuimarisha demokrasia na kuimarisha afya ya jamii na kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.

Alisema kuwa nchi yake iko tayari kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika Nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vya ufundi VETA ambavyo alisema ni muhimu katika maendeleo ya nchi na kwamba uwekezaji unaofanywa na mashirika na taasisi mbalimbali nchini unahitaji nguvu kazi yenye ujuzi.

Akiwa nchini, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, kutoka Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mhe. Dkt. Barbel Kofler, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Maliasili na Utalii, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Katiba na Sheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.