Habari za Punde

Wakulima na Wafugaji Wanaoshiriki Maonesho ya NaneNane Kuitumia Vyema Fursa Hii Kutafuta Elimu ya Matumizi Sahihi ya Zana za Kisasa- Dk Mwinyi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakichuma Karafuu katika Kitalu cha Maonesho cha Kilimo cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) baada ya kuyafungua Maonesho ya Nanenane Viwanja vya Kizimbani Wilaya ya Magharibi "A" Unguja leo 8-8-2022.
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza wakulima na wafugaji wanaoshiriki Maonyesho ya Nane nane kuitumia vyema fursa hiyo kutafuta elimu  ya matumizi sahihi ya zana za kisasa, mbegu bora na pembejeo ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo na Ufugaji nchini.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika Ufunguzi wa Maonesho ya kilimo Nane nane yaliofanyika Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema wakulima na wafugaji wanapaswa kuyatumia maonesho hayo katika kutafuta elimu inayohusu matumizi ya zana za kisasa, upatikanaji wa mbegu bora, elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na njia za kupambana na maradhi yanayoathiri sekta hizo.

Alisema kuwepo kwa maonesho hayo kunatoa fursa kwa wananchi kuona mbinu za kisasa za kilimo, ufugaji, uvuvi pamoja na shughuli mbali mbali za kibiashara na ujasiriamali.

Aidha, alisema maonesho hayo yanatoa fursa ya kuwakutanisha ana kwa ana wadau mbali mbali, wakiwemo wazalishaji na wateja wao, hatua inayotoa mchango mkubwa katika kukuza na kuongeza ubunifu, kutambua mafanikio, changamoto pamoja na upatikanaji wa masoko.  

Akigusia Kauli mbiu ya Maonesho hayo isemayo ‘Kilimo ni Biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya sekta ya Kilimo’ Dk. Mwinyi alisema kaulimbiu hiyo imekuja kwa wakati muafaka kwa kuzingatia  changamoto kadhaa zinazoikabili Dunia na kutishia kuathiri hali ya Usalama wa Chakula.

Alisema sekta zote za uzalishaji na usafirishaji zimeathirika kutokana na janga la Uviko 19 pamoja na mgogoro ulioibuka baina ya Mataifa ya Urusi na Ukrane; mataifa yenye mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula,hususan ngano pamoja na uzalishaji wa mbolea na pembejeo.

Alisema athari hizo zimeifanya Serikali kupunguza ushuru na kufidia bei za bidhaa muhimu na hivyo kuathiri kiwango cha ukusanyaji mapato na kuongezeka kwa matumizi.

Dk. Mwinyi alisema Wizara Kilimo, Umwagiliaji, Maliasi na Mifugo ina jukumu la kuwa na mikakati madhubuti itakayoliwezesha taifa kuongeza uzalishaji na kuondokana na utegemezi wa bidhaa za chakula kutoka nje.

Alisema ni muhimu kuendeleeza kilimo cha kisasa kwa kuwashajiisha makundi ya vijana kujishughulisha na sekta ya kilimo ili kuiongeza mchango wake na kukuza ajira.

“Wito wangu tuendelee kuyaimarisha mfafanikio  tuliopata kwa kuwashajisha vijana  wengi zaidi kushiriki katika sekta ya kilimo kwa kuwapatia vifaa vya kisasa, mbegu bora na taaluma juu ya matumizi bora na sahihi ya pembejeo”, alisema.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwakumbusha wakulima na wananchi kuongeza uzalishaji wa bidhaa za matunda na bidhaa nyingine zitokanazo na Uvuvi kwa kigezo cha kuwepo mahitaji makubwa Mahotelini, wakati huu bidhaa hizo zikiagizwa kutoka nje ya nchi.

Akizungumzia uzalishaji wa zao la Mpunga Dk. Mwinyi alisema Serikali inashirikiana na wadau mbali mbali kuendeleza kilimo cha zao hilo kwa njia ya Umwagiliaji maji, ambapo jumla ya hekta 1,053 zinaendelezwa katika mabonde mbali mbali Unguja na Pemba.

Alitumia fursa hi#yo kuwahimiza wakulima watakaopata Vitalu katika mabonde hayo kuvitunza na kuviendeleza ili lengo la Serikali la kuendeleza miradi mikubwa ya umwagiliaji maji kuona inafanikiwa.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kushajiisha Wawekezaji kuwekeza kwenye sekta ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na kuzifanyia kazi changmoto ziliopo za upatikanaji wa mbegu bora, vifaranga pamoja na chakula cha mifugo.

Alisema kazi hiyo inapaswa kwenda sambamba na juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira, ikiwa pamoja na kulima na kuhifadhi maliasili za misitu, ikiwemo mikoko.

“Tushirikiane kuyalinda na kuyatumia vizuri maeneo yaliotengwa kwa shughuli za kilimo na kuendelea kuhimizana juu ya upandaji miti ya matunda na ile ya asili”, alisema.

Aidha, Dk. Mwinyi alirudia kauli yake ya kusisitiza umuhimu wa kuendeleza kilimo cha Mikarafuu ili kuongeza uzalishaji, akibainisha kuwa na umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Uchumi wa Zanzibar.

Aliipongeza Uongozi wa Serikali Awamu ya saba kwa kuja na mpango maalum wa miaka 10 wa kufufua zao hilo, na kutilia mkazo upandaji wa miche mipya, ushughulikiaji mashamba, kutoa mikopo pamoja na Bima kwa wakulima.

Aliuagiza Uongozi wa Wizara Kilimo, Umwagiliaji, Maliasi na Mifugo kushirikiana na Shirika la Biashara (ZSTC) , pamoja na Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuongeza kasi ya upandaji wa mikarafuu mipya, akibainisha kuwepo maeneo mengi katika kisiwa cha Unguja ambayo zao hilo hustawi na bado hayajatumika ipasavyo.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi  aliitaka Wizara hiyo kuwa na mipango imara na endelevu ya kuzalisha miche ya miti ya matunda na miti ya asili na kuigawa bure kwa wakulima  katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba

Aidha, aliitaka Wizara hiyo kuongeza kasi katika kufanya tafiti mbali mbali za kilimo na baadae kusambaza matokeo yake, sambamba na na kushajiisha matumizi ya tafiti hizo kwa wadau.

“Serikali imeanzisha taasisi ya Kilimo na taasisi nyingine za Mifugo ili zituwezeshe kuondokana na  changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta hiyo”, alisema.

Alibainisha kuwa tafiti hizo zinahitajika ili kupata mbegu bora na kupambana na maradhi, pamoja na wadudu waharibifu wa matunda.

Nae, Waziri wa Wizara Kilimo,  Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Shamata Shaame Khamis aliihakikishia Serikali kuwa maelekezo na miongozo inayotowa itashughulikiwa na kusimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha kunakuwepo upatikanaji wa uhakika wa chakula hapa nchini.

Alisema maonesho hayo yameweza kufanikiwa kufanyika kutokana na mashirikiano makubwa kati ya Wizara hiyo na wadau mbali mbali, bila ya kuwepo matumizii ya fedha za bajeti ya Serikali.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo  Seif Shaaban Mwinyi alisema Maonesho hayo yamewashirikisha Wajasiriamali 155 kutoka Taasisi 52, ambapo jumla ya shilingi Milioni 78 zimetumika hadi sasa, kutokana na michango  na ahadi  kutoka kwa wadau mbali mbali.

Alisema azma ya Wizara hiyo ni kulizungushia uzio eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 9.4 ili liweze kutumika kwa shughuli za maonesho muda wote.

Katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, apata fursa ya kutembelea Mabanda mbali mbali  na kuangalia bidhaa mbali mbali zinazozalishwa an Wakulima na wafugaji.

Aidha, Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki katika hafla hiyo, akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.