Habari za Punde

Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake ili sekta ya elimu nchini izidi kuimarika pamoja na kuwa na mazingira bora ya kufanyakazi kwa walimu wake.

 

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe.Rajab Yussuf Mkasaba akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Paje Zanzibar Mhe. Jafar Sanya Jussa alipowasili katika viwanja vya Skuli ya Jambiani kuhudhuria Mahafali ya Skuli hiyo ya Watahiniwa wa Kidato cha Nne.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja akimkabidhi Cheti mmoja wa Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Jambiani wakati wa hafla ya kukabidhiwa Vyeti Watahiniwa wa Kidatu cha Nne wa Kada Maalum ya michezo ambayo ndio skuli ya pekee katika Mkoa wa Kusini Unguja inayofundisha kada hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja akimkabidhi Cheti mmoja wa Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Jambiani wakati wa hafla ya kukabidhiwa Vyeti Watahiniwa wa Kidatu cha Nne wa Kada Maalum ya michezo ambayo ndio skuli ya pekee katika Mkoa wa Kusini Unguja inayofundisha kada hiyo.
Mwanafunzi  Fadhil Murid Rajab akionesha kipaji chake cha utangazaji wakati wa hafla ya Mahafali ya Kidato cha Nne kwa Wanafunzi Watahiniwa wa Skuli ya Jambiani Wilaya ya Kusini Unguja 


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane inathamini jitihada kubwa zinazofanywa na walimu nchini na ndio maana imewapandishia kiwango cha mishahara ili kuwatia hamasa na kuwasaidia katika kuendeleza maisha yao sambamba na kuleta matokea chanya kwa wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Rajab Yussuf Mkasaba aliyasema hayo katika Mahafali ya Nne ya kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaotarajiwa kufanya mitihani yao mwezi ujao  katika Skuli ya Sekondari ya Jambiani iliyopo Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika maelezo yake Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini aliahidi kwamba Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake ili sekta ya elimu nchini izidi kuimarika pamoja na kuwa na mazingira bora ya kufanyakazi kwa walimu wake.

Aliwanasihi walimu wa skuli ya Sekondari Jambiani kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili skuli hiyo iendelee kutoa wahitimu wenye uwezo wa hali ya juu kitaaluma na kuondokana na ile dhana ya kwamba skuli za Wilaya hiyo zimekuwa hazifanyi vizuri katika mitihani ya Taifa.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini alieleza juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika ikiwa ni pamoja na kutoa fedha nyingi kupitia fedha za UVIKO -19 katika ujenzi wa skuli mpya za kisasa Unguja na Pemba.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya huyo alitumia fursa hiyo kutoa pongezi maalum na shukurani kwa wale wote wanaoendelea kuiunga mkono skuli hiyo kwa lengo la kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika katika Wilaya hiyo.

Mkasaba alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msaada wa chakula yakiwemo magunia kumi ya mchele, vyakula vyengine, vifaa na magodoro kwa ajili ya wanafunzi wanaokaa kambi wakijiandaa na mitihani katika skuli zote za Sekondari za Wilaya hiyo.

Pia, aliwakumbusha wanafunzi ambao wanajitayarisha na mitihani ya Kidato cha Nne ambao wameagwa rasmi katika hafla hiyo kutambua kwamba kumaliza kwao ngazi waliofikia ya taaluma ni mwanzo wa ngazi inayofuata.

“Wazee walisema Elimu haina mwisho, kwa hivyo mnapaswa kujiandaa kwa ngazi ya taaluma inayofuata”, alisema Mkasaba.

Sambamba na hayo, aliwanasihi wanafunzi wanaoendelea na masomo yao katika skuli hiyo ya Sekondari Jambiani kuwa na bidii katika masomo na kujifunza siri za mafanikio ambayo wameyapata ndugu zao wanaotarajia kufanya mitihani yao ya Kidato cha Nne mwezi ujao.

Akieleza hatua zilizochukuliwa na Wilaya hiyo katika kupambana na changamoto zilizoelezwa na wanafunzi hao katika risala yao ikiwemo suala zima la upigaji ngoma na miziki alitoa ufafanuzi juu ya kadhia hiyo alieleza kwamba tayari Ofisi yake imeazimia kuwakumbusha wamiliki wote wa hoteli pamoja na Baa za Wilaya hiyo kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni (BASSFU).

Alisisitiza kwamba kwa kipindi hichi chote ambacho wanafunzi wanajiadaa na mitihani yao ikiwemo ya darasa na Nne, Darasa la Saba, Kidato cha Pili pamoja na Kidato cha Nne hairuhusiwi kupigwa ngoma ya aina yoyote katika hafla zote mpaka pale mitihani itakapomalizika.

Nao wahitimu watarajiwa wa Kidato cha Nne wa skuli hiyo katika risala yao walieleza kwamba elimu waliyoipata ya Kidato cha Nnne imewapa misingi imara ya kujiunga na Elimu ya Juu pia, kuwajengea uwezo wa kujitambua na kufikiria kabla ya maamuzi.

Katika hafla hiyo Mkuu huyo wa Wilaya aligawa vyeti maalum kwa wanafunzi wa Michezo pamoja na kushuhudia sanaa mbali mbali zilizotumbuizwa na  wanafunzi wa skuli hiyo ikiwemo utenzi, nashid, mashindano ya kukuna nazi pamoja na kipaji kilichooneshwa na mwanafunzi mwenye mahitaji maalum wa skuli hiyo.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Mwakilishi, Mbunge pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja.

Imetayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini,

Mkoa wa Kusini Unguja.

21.10.2022.

 

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.