Na Shamimu Nyaki
Serikali ya Afrika Kusini
imetoa pongezi na shukrani kwa Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi na kulinda
maeneo ya Historia ya wapigania Uhuru wa nchi hiyo yaliyoko Mazimbu mkoani
Morogoro.
Pongezi na Shukrani hizo
zimetolewa na Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini,
Mhe. Nocawe Mafu wakati alipozungumza katika mdahalo wa mashuhuda wa wapigania
Uhuru wa nchi hiyo, ikiwa ni siku ya pili ya Tamasha la Afrika Kusini
linaloendelea nchini Novemba 19, 2022.
"Afrika Kusini na
Tanzania ni ndugu, tumeshuhudia jinsi mnavyoenzi undugu huu, tumefurahi kuona
mnavyotunza na kulinda maeneo ya Urithi wa Ukombozi wa Bara letu zaidi nchi
yetu, nawaahidi makubaliano ya ushirikiano wetu yote tutayatekeleza",
amesema Mhe. Nocawe.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya
Morogoro, Mhe. Alberto Msando akiwasilisha salamu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, amesema kuwa nchi hizo
zinashirikiana katika Sekta nyingi ambapo waasisi wa nchi hizo Baba wa Taifa
Hayati Julius Nyerere na Nelson Mandela walihakikisha nchi hizo zinakuwa huru
na pamoja na Bara zima la Afrika.
Mhe. Msando alitumia nafasi
hiyo kuwaongoza Naibu Waziri huyo, Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini, Mhe.
Nolurthando Malepe na Raia wa Taifa hilo kutembelea Kambi ya wapigania Uhuru wa nchi hiyo pamoja
na makaburi waliozikwa Mashujaa waliopigania Uhuru wa Taifa hilo.
Ziara hiyo ni katika siku ya
pili ya Tamasha la Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania wenye lengo la
kuimarisha uhusiano katika Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni sehemu
ya utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Utamaduni uliosainiwa
mwaka 2011.

No comments:
Post a Comment