Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis (kushoto) akishiriki katika mjadala ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu jitihada za Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni sehemu ya mijadala katika Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Sharm El-Sheikh, Misri.
Serikali
kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi
na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2032)
kwa lengo la kutoa mwongozo wa hatua za kuchukua ili kutatua changamoto za
mazingira nchini kwa kuzingatia upekee wa changamoto katika sehemu husika na
hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Khamis Hamza Khamis leo wakati wa mjadala ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu
jitihada za Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni
sehemu ya mijadala katika Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa
kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Sharm El-Sheikh, Misri.
Amesema
mpango kambambe huo unaonesha changamoto za mazingira zinazoikabili Tanzania
ikiwa ni pamoja na uharibifu wa ardhi; uharibifu wa vyanzo vya maji; athari za
mabadiliko ya tabianchi; uchafuzi wa mazingira; ukataji ovyo wa miti na
uharibifu wa misitu; upotevu wa makazi ya wanyamapori na bioanuai.
“Uharibifu
wa mfumo-ikolojia ya pwani na baharini; uharibifu wa ardhi oevu; usimamizi
hafifu wa taka; kuenea kwa viumbe vamizi; na changamoto za mazingira katika
miji zimeanishwa katika Mpango huo,” alisisitiza Naibu Waziri Khamis.
Amesema
Mpango Kambambe unatoa hatua za kimkakati na mahsusi kwa kuzingatia jiografia
na mifumo ikolojia ya maeneo husika. Hatua hizo zinazingatia utofauti wa
mtawanyiko wa changamoto za mazingira na hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa
na kutoa mwongozo kuhusu usimamizi wa mazingira.
Naibu Waziri Khamis amesema kupitia ufadhili wa shirika la
Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Uendelezaji Mitaji (LoCAL),
serikali imeanza kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi katika halmashauri tatu za
Kondoa, Chamwino na Mpwapwa pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi wa kuhuisha
masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Ametoa wito kwa jamii kuhakikisha zinaendelea kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kuwa Mabadiliko ya Tabianchi ni halisi na kusisitiza utekelezaji wa Sera na Mikakati kwa pamoja kwa kesho iliyo bora kwa kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Itakumbukwa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya
Mazingira ulizinduliwa Juni 5, 2022 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis (kushoto) akishiriki
katika mjadala ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu jitihada za Tanzania
katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni sehemu ya mijadala
katika Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa
Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Sharm El-Sheikh, Misri.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis (kulia) akimkaribisha
Mhandisi Steven Mlote Naibu Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki
(anayeshughulikia masuala ya Miundombinu, Mipango, Fedha na Utawala) katika
Banda la Tanzania katika Mkutano wa 27 wa Nchi
Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Sharm
El-Sheikh, Misri. Mhandisi Mlote ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada
za kukabilina ana athari za mabadiliko ya tabianchi na uwekezaji katika miradi
ya kimkakati.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis (kushoto) akizungumza na Bi. Rachel Kennedy mmoja ya wawezeshaji katika mjadala ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu jitihada za Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni sehemu ya mijadala katika Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Sharm El-Sheikh, Misri.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
No comments:
Post a Comment