Habari za Punde

Ruaha CDTI Watumia Milioni Mia Sita kwa Ujenzi wa Majengo Manne

Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia,wanawake na makundi maalumu Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwapongeza chuo Cha maendeleo ya Jamii Ruaha mkoani Iringa Kwa mapambano dhidi ya udumavu na utapiamlo.
Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha (CDTI, Godfrey Mafungu akiongea na wahitimu pamoja na wageni waalikwa juu ya maendeleo ya chuo hicho

Na Fredy Mgunda,Iringa.

CHUO cha Maendeleo ya Jamii Ruaha (CDTI) kilichopo mkoani Iringa kimeanza Kutekeleza taratibu za awali za kufanya utafiti wa hali ya Lishe na Udumavu katika Manispaa ya Iringa na kimeanzisha Dawati la Jinsia kwa ajili ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia lengo likiwa ni kupunguza udumavu na kuondoa ukatilii kwa jamii.

 

Akizungumza wakati wa mahafali ya chuo Maendeleo ya Jamii Ruaha (CDTI,mkuu wa chou hicho Godfrey Mafungu alisema kuwa chuo hicho kimefanikiwa kujenga ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanachuo 260, Mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanachuo 128 na maktaba yenye uwezo wa kuchukua wanachuo 144 kwa awamu moja

 

Mafungu alisema kuwa wameanza utekelezaji wa programu ya Ushirikishwaji jamii,Uanagenzi na kituo cha ubunifu na maarifa ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ibara 229 na uwepo wa miradi ya uzalishaji mali kwa lengo likiwa ni kutoa mafunzo na kuongeza mapato ya ndani ya Chuo.

 

Alisema kuwa katika kuendelea kuboresha miundombinu ya chuo ili kuwezesha kutoa huduma bora za mafunzo kwa wanachuo,serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum ilikipataia chuo kiasi cha shilingi za kitanzania milioni mia sita (600,000,000.00) kuweza kutekeleza miradi ya ujenzi wa majengo manne.

 

Mafungu alisema kuwa ujenzi wa ukumbi wa mihadhara (Lecture Hall) unaogharimu shilingi za kitanzania milioni mia moja (100,000,000.00) mpaka kukamilika kwake na ina uwezo wa kuchukua wanachuo 260 kwa awamu moja, Ujenzi wa Maktaba ya kisasa unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni mia mbili (200,000,000.00) na kuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 144 kwa awamu moja na Ujenzi wa mabweni mawili unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni mia tatu (300,000,000.00) ikiwa shilingi milioni mia moja hamsini (150,000,000.00) kwa kila moja na uwezo wa kuchukua wanachuo 128 kwa awamu moja kwa majengo yote mawili.                                               

 

Kwa upande wake mgeni rasmi katika mahafali hayo Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia,wanawake na makundi maalumu Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amepongeza chuo Cha maendeleo ya Jamii Ruaha mkoani Iringa Kwa mapambano dhidi ya udumavu na utapiamlo.

 

Akitoa pongezi hizo Leo wakati wa Mahafali ya 14 ya chuo hicho Naibu Waziri huo amesema jitihada kubwa zimefanywa na chuo hicho Katika utoaji elimu ya lishe Kwa jamii inayozunguka.

 

Hata hivyo amepongeza menejimenti ya chuo Kwa kuendelea kuimalisha Mapato ya ndani Kwa kubuni vyanzo vya Mapato kama ugugaji samaji,uchakataji ngozi na shughuli nyingine za Kiuchumi.

 

Alisema alipofika chuoni hapo alitembelea mabwawa ya samaki na kuona jitihada hizo kubwa ambapo kupitia ugugaji huo wananchi watapata Afya Bora.

 

Aidha waziri Khamis alipongeza chuo Kwa kupata kibali Cha utafiti wa lishe Iringa na kuagiza vyuo vingine kuandika maandiko ya kazi mbali mbali za chuo Kwa lengo la Kutangaza chuo.

 

Akielezea changamoto za chuo hicho kama Nyumba za walimu na Mabweni alisema changamoto hizo amezichukua na atakwenda kuzifanyia kazi kwa kuwa suala la miundo mbinu ya barabara atauagiza uongozi wa mkoa ili kuboresha mazingira ya chuo hicho.


waziri Khamis aliwataka wahitimu wa chuo hicho kutumia vema mafunzo ambayo wamepata Kwa kwenda Vijijini kuwatumikia wananchi kama ambavyo Rais  Samia Suluhu Hassan ameunda wizara ya maendeleo ya Jamii ili kusaidia jamii kupata elimu Bora .

 

"Ndugu wahitimu mtakapopata fursa ya kupata kazi jiepusheni na vitendo vya Rushwa na miawe mabalozi mazuri wa kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia"

 

"Tumekuwa tukifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na nimekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za Chuo katika utekelezaji wa majukumu yake, ninaahidi kutimiza wajibu wangu nikiwa kama Naibu Waziri, kwa kutoa msaada pale itakapohitajika na nitakapoona inafaa".

 

Alisema anatambua kuwa ili kuweze kufikia malengo waliyojiwekea katika kutekeleza mpango mkakati wa Chuo, ni lazima kuwe na juhudi za makusudi za kuhakikisha upatikanaji wa fedha za maendeleo.

 

" Nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kwa kushirikiana na Wizara yetu pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha suala la upatikanaji wa fedha za kutosha za ruzuku na miradi ya maendeleo kwa ajili ya uendeshaji wa Chuo hiki linapewa kipaumbele Ndugu Wahitimu, Napenda nitumie fursa hii kuwapongeza sana wote ambao mtatunukiwa hivi punde Stashahada na Astashahada za Maendeleo ya Jamii. Niwapongezeni sana kwa juhudi kubwa mliyoonyesha katika kipindi chote mlichokuwa hapa Chuoni,kilichowapelekea kufikia mahafali ya siku ya leo"  


Alisema anatambua umuhimu wa elimu ya Maendeleo ya Jamii katika maendeleo ya ulimwengu wa sasa; napenda niwasisitize umuhimu wa kujiendeleza katika fani hii ili muweze kuwa chachu ya mabadiliko chanya ya kimtazamo wa jamii. 


Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anachukizwa Sana na vitendo vya ukatili vinavyojitokeza Katika jamii yetu hivyo ni jukumu lenu kwenda kulifanyia kazi janga la ukatili Kwa kutoa elimu Bora na wale wanaopata msongo wa mawazo Kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili mkawasaidie kuwapa elimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.