Tanzania
imekamilisha maandalizi ya Mkakati wa Kitaifa wa Kurejesha Mandhari ya Misitu
wenye lengo la kuongoa ardhi iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa
niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mhe. Mohamed Soud aliyetaka kujua Kampeni ya
AFR imetekelezwa kwa kiasi gani.
Amesema
mkakati huo unatarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa
kujadili masuala ya Mazingira unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 30,2022
nchini Misri.
Sambamba
na hilo amesema Serikali imesaini makubaliano ya Kurejesha Mandhari ya Kiafrika-
kupitia kampeni ya AFR 100 iliyokuwa na adhma ya kuongoa hekta milioni 100 za
ardhi iliyoharibiwa barani Afrika.
Kupitia
kampeni hiyo Tanzania iliahidi kuongoa hekta milioni 5.2 za ardhi iliyoharibiwa
ambapo kwa sasa inatekelezwa kwa Kuondoa wavamizi na kurejesha ardhi
iliyoathiriwa, kuimarisha usimamizi wa misitu ya mikoko, kutoa elimu ya
kudhibiti moto wa msituni ili kulinda uoto wa asili na kutekeleza Mpango wa
Dodoma ya Kijani.
Awali,
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Antropia Theonist kuhusu
waathirika wa wanyama wakali katika Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Masanja ametoa pole
kwa wananchi walioathirika na wanyama hao na kusisitiza kuwa Serikali
itaendelea kufanyia kazi suala la kifuta jasho/machozi.
No comments:
Post a Comment