Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe.Ayoub Mohammed Akanusha Taarifa ya Ajali ya Moto Kuwa Sio ya Ukweli

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud alipokua akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na uvumi wa  tukio la moto linalosambaa  mitandaoni likionyesha kuungua kwa  Hoteli za Nungwi ,huko Ofisini kwake Mkokotoni Kaskazini Unguja.
(PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR)

Na.Rahma Khamis Maelezo        26/2/2023

Jamii nchini imetakiwa kuacha kusambaza taarifa zisizo na uhakika katika mitandao ya kijamii ili kuepusha taharuki kwa wananchi.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu uvumi uliyotolewa siku ya Alhamis katika mitandao ya kijamii kuhusiana na  kuungua kwa Hoteli tatu za Nungwi huko Ofisini kwake Mkokotoni, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Muhamed Mahmoud amesema taarifa hizo si za kweli na zina lengo la kupotosha jamii na kuwatia hofu wageni wanaotaka kuja kutembelea Zanzibar.

Amesema kitendo cha kusambazwa kwa taarifa hizo ni kwenda kinyume na sharia za matumizi ya mtandao hivyo ipo haja kwa wahusika kutafuta chanzo cha taarifa hiyo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha amefahamisha kuwa kuenea kwa taarifa hizo katika Mkoa wa Kaskazini kunapelekea baadhi ya wageni kuona kwamba Mkoa huo hauko salama jambo ambalo linakosesha ongezeko la pato la taifa.

Hata hivyo Mkuu huyo ametoa wito kwa wamiliki wa Hoteli na wananchi kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari hasa wakati wa kiangazi ili kujilinda na ajali za moto.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.