SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar imesema inathamini juhudi za taasisi binafsi katika
kuisaidia serikali kuwafikishia wananchi huduma za jamii zikiwemo afya, elimu,
maji na umeme.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo Ikulu,
Zanzibar alipozungumza na uongozi wa Jumiya ya Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania
waliofika kuzungumza naye.
Dk. Mwinyi alisema
Serikali inaungamkono juhudi njema zinazofanywa na taasisi za dini kusaidia
kuleta maendeleo ya nchi pamoja na kuendelea kuitangaza amani.
Aliishukuru taasisi hiyo
kwa misaada wanayoitoa kwa jamii na kueleza serikali daima iko pamoja na taasisi
zinazoungamkono juhudi za Serikali.
“Kipekee
niishukuru taasisi yenu kwa misaada mnayoitoa kwa jamii, sisi kama serikali
tuna wajibu wa kutoa huduma za jamii kwa wananchi lakini wakati mwengine
hatuwezi kufanya hayo yote hutokana na uwezo wa Serikali zetu, idadi ya watu na
ukubwa wa nchi, hivyo mara zote tunawashukuru wale wanaotuungamkono”. Alieleza
Dk. Mwinyi.
Alisema
thamani kubwa ya nchi ni kudumisha amani, na yeyote anayeihubiri amani na kujitihadi
kuidumisha lazima Serikali imuunge mkono kwa kutambua umuhimu wa amani katika
ustawi wa nchi.
Alieleza
Serikali inawataka wananchi wote waendelee kuimarisha umoja, upendo na kuvumiliana.
Hata hivyo alieleza serikali haibagui taasisi yeyote iwe ya dini, siasa au
jamii muhimu itii sheria za nchi na taratibu zake.
Akizumgumza Amiiri
na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh
Tahir Mahmood alisema Tanzania inasifika kwa amani, umoja na mshikamo wa watu
wake nakueleza mara zote, serikali zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania nay a Mapinduzi ya Zanzibar zinajali uhuru wa kuabudu licha ya kuwepo
kwa imani tofauti za dini, lakini wanaendelea kuishi kwa umoja jambo
alilolieleza kwamba ni mafanikio makubwa kwa taifa.
Naye, Naibu Amir wa
taasisi hiyo, Sheikh Abdul Rahman Muhammad Ame alieleza taasisi hiyo ilitoa
mchango mkubwa kwa taifa tokea kuanzishwa kwake mwaka 1934, kwa baadhi ya
waumini wake kina Marehemu Sheikh Kaluta Amri Abedi, Mzee Hassan Tawfiq na
wengine walishirikiana na Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere
kwenye harakati za ukombozi na kuleta uhuru wa nchi.
Alisema taasisi ya Ahmadiyya
Muslim Jamaat ilikua ya kwanza kuchapisha kadi za chama cha TANU kwa wakati huo
kupitia mtambo wa jumuiya hiyo uliokuwepo Tabora ukichapisha gazeti la
Kiswahili la jumuiya lililoitwa “Mapenzi ya Mungu”.
Aliongeza jumuiya hiyo
ndio iliyobuni jina la “Tanzania” kupitia muumini wake bw. Muhammad Iqbal Dar
aliekua akiishi Morogoro kwa wakati huo. Pia alieleza jumuiya hiyo ilikua ya
kwanza kuitafsiri Quran kwa lugha ya kiswahili pamoja na kutoa mchango mkubwa
wa kukuza Kiswahili, Afrika Mashariki baada ya kuchapisha gazeti la Kiislam kwa
lugha ya hiyo ambalo alisema lilitoa hamasa kubwa wakati wa harakati za
ukombozi kupitia Makala na mashairi.
Taasisi ya Ahmadiyya
Muslim Jamaat Tanzania ni Jumuiya ya kimataifa yenye malengo ya kidini, ipo
kwenye nchi 212 duniani kote na sasa ina zaidi ya waumini 50,000 Tanzania na
imesaidia huduma za jamii kujenga vituo vya afya, maji, umeme wa jua na elimu
vijijini. imeongozwa na Makhalifa wanne na watano ni Sheikh Hadhrat Mirza
Masroor anaendea kuongoza hadi sasa.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment