Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Atembelea Bandari ya Malindi Zanzibar

Muonekano wa Bandari ya Malindi Zanzibar ikiwa katika harakati za kushusha makontena katika bandari hiyo kama inavyoonekana wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla 
Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe.Dkt. Khalid Salum Mohammed akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla , katika bandari ya Malindi Zanzibar. 



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amelipongeza Shirika la Bandari Zanzibar kwa kupunguza  changamoto ya msongamano wa Makontena Bandarini.

Mhe. Hemed ameyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua shughuli za  ushushaji wa Makontena Bandari ya Malindi pamoja na kukagua  maeneo yanayowekwa makontena katika Bandari kavu ya Bwawani na Maruhubi Jijini Zanzibar.

Amesema ni hatua ya kufurahisha kuona Shirika hilo limetenga maeneo ya kuweka Makontena kwa mujibu wa mchanganuo wake ili kupunguza mrundikano Bandarini.

Amesema ni vyema kwa Taasisi husika kuweza kushirikiana pamoja ili kurahisisha huduma kwa wafanayabiashara kutokaa muda mrefu bandarini kwa mujibu wa Sheria.

Aidha amewataka watendaji wa Shirika la Bandari kufanya kazi masaa Ishirini na Nne (24) ili kupunguza siku za kukaa meli Bandarini.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameutaka Uongozi wa Shirika hilo kuhakikisha kila Mfanyabiashara anaedaiwa kwa kuchelewa kutoa Makontena analipa kwa mujibu wa sharia.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  amesema uharakishwaji wa utoaji wa Makontena Bandarini utasaidia kuiongezea Serikali mapato na kuweza kuwashawishi wafanyabiashara wengine kuongeza idadi ya Meli na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa nchini.

Katika Ziara hiyo Mhe. Hemed ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi kulitoa Kontena moja lenye  Mchele Mbovu kati ya Makontena matano lililobaki Bandarini na kuchukua hatua stahiki kisheria ikiwa kuurejesha ama kuuangamiza.

Nae Waziri wa ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Dkt. Khalid Salum Muhamed ameeleza kuwa Wizara kupitia Shirika la Bandari limetatua changamoto zilizokuwa kikwazo bandarini hapo ikiwemo Vifaa vya kushushia kontena, eneo la kuweka makontena yenye mizigo, pamoja na eneo la kuweka makontena matupu.

Aidha amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kukaa pamoja na uongozi wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ili watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania waweze kuhamia eneo la Malindi kurahisisha upakuaji wa Makontena.

Nae Mkurugenzi  Mtendaji wa wa Shirika la Bandari Zanzibar Ndugu Nahat Muhamed Mahfoudh ameeleza kuwa Shirika tayari limenunua mashine za kushushia Makontena ili kuongeza ufanisi wa kazi.

Aidha Ndugu Nahat ameeleza kuwa Shirika limeweka ulinzi wa kutosha eneo la bandari kavu Bwawani na maruhubi ili kuweka usalama wa Makontena yanayowekwa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.