Habari za Punde

Serikali kuzingatia mafungu maalum ya fedha kwa waviu katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Mwalimu Leticia Mourice baada ya kumaliza Mazungumzo hayo.

 

NA; MWANDISHI WETU - DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, amesema utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na vipaombele vingine inazingatia pia mafungu ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) katika kila Wizara na Taasisi.

Ameyasema hayo mapema leo 25 Mei 2023, katika Ukumbi wa Waziri Mkuu Bungeni Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA).

Mhe. Mhagama, aliendelea kusema kuwa hii ni namna ambavyo Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kwa dhati kusaidia utekelezaji wa Afua za masuala ya UKIMWI nchini, kwa kuzingatia maeneo muhimu ikiwemo masuala ya lishe bora, dawa za kupunguza makali ya virusi na kuhakikisha mambo mengine yanayochangia ustawi wao kupatikana.

Akizungumzia suala la Sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001 Mhe. Mhagama alisema kuwa kuna kila Sababu ya Sera hiyo kufanyiwa mapitio na maboresho kwani ni ya muda mrefu na kuona, namna gani sekta zote zinaweza kushiriki katika suala hili ili kuweza kuyafikia malengo ya dunia ya kupunguza vifo, maambukizi na unyanyapaa ifikikapo 2030.” Niwahakikishie kwamba sisi kama Serikali tunaweza kusimamia kufikia malengo haya ya dunia”Alisisitiza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa NACOPHA Mwalimu Leticia Mourice alimpongeza Mhe. Waziri Jenista kwa uteuzi wake na pia kumshukuru kwa juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI, aidha aligusia kuhusiana na maandalizi ya Mdahalo wa Kitaifa kuhusu uhimilivu wa mwitikio wa jamii katika mwitikio wa Taifa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Sambamba na hilo alizungumzia kuhusu, uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Taifa, ambao unalenga utekelezaji wa NMSF5 (Mpango Mkakati wa Tano wa Kitaifa wa Kudhibiti UKIMWI) na alisisitizia umuhimu wa ushirikiano, katika kujenga mwitikio wa kijamii katika mapambano dhidi ya UKIMWI, akitolea mfano maeneo kadhaa muhimu ikiwemo Uhimilivu wa Kisera.

Awali, akizungumza katika mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA Bw. Deogratius Rutatwa, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuipongeza Serikali ya watu wa Marekeni (PEPFAR/USAID) kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha shughuli za mwitikio wa UKIMWI za NACOPHA na wadau wote wanaotekeleza suala la UKIMWI na kusema kuwa kuna haja ya kuwepo kwa mkakati endelevu na uhimilivu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) katika Ukumbi wa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma 
Afisa Mtendaji Mkuu kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Bw. Deogratias Rutatwa akitoa maelezo kuhusu NACOPHA kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani).
Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Nchini na mjumbe wa Bodi ya NACOPHA Bi. Pudensiana Mbwiliza akitoa maelezo namna ya vijana hao wanavyonufaika na NACOPHA wakati wa kikao chao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe Jenista Mhagama.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Sera na Programu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Crispin Musiba akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.

Baadhi ya Wajumbe waliohudhuria kikao hicho wakifuatilia hoja.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.