Habari za Punde

Wizara ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA Yajipanga kuhakikisha Mawasiliano Yanakuwa na Tija Kwa Watanzania

 

Na Innocent Mungy, Arusha.                                                                                             

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imedhamiria imejipanga kimkakati katika mwaka wa Fedha wa 2023/2024 kuleta mabadiliko makubwa ya huduma za Habari, Mawasiliano na TEHAMA nchini zenye tija kwa watumiaji wote nchini.

Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, wakati wa akifunga Kikao Kazi cha Viongozi wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake. Mheshimiwa Nape alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Wizara itatekeleza mambo makubwa matano ambayo yataboresha huduma za mawasiliano nchini na kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma hizo nchini.

Akitaja jambo la kwanza alisema, “Nimezindua Kamati ya Ushauri ya Masuala ya Kiseramajuzi. Kamati hiyo inasimamiwa na mimi mwenyewe na wajumbe wa Kamati hii ni Wenyeviti wa Bodi zote za Taasisi zilizo chini ya Wizara. Lakini ipo Kamati Tendaji ambayo itaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara na hii wajumbe wake ni Wakuu wote wa Taasisi zilizo chini ya Wizara. Hali kadhalika kutakuwa na Kamati ya Wataalamu ambayo wajumbe wake ni Wakurugenzi wa Wizara na wale wa Taasisi zilizo chini ya Wizara watakaowajibika kuishauri Kamati Tendaji. Kamati hii itaongozwa na Naibu Katibu Mkuu. Kamati hizi zinakwenda kufanya kazi kubwa ya kuleta mabadiliko makubwa kwenye Sekta” alisema Mhe. Nape.

Jambo la pili alisema ni Wizara kukamilisha Mkakati Mawasiliano wa Taifa kwa Umma. “Kuna ombwe kubwa la uratibu wa shughuli za mawasiliano Serikalini. Serikali imeona tatizo hilo na jinsi masuala ya Mawasiliano yanavyofanyika hasa wakati wa dharura. Tunaenda kukamilisha Mkakati huu na kuanza kuutekeleza katika mwaka huu wa Fedha wa 2023/2024” alisema Mhe. Nape.

Akizungumzia jambo la tatu, alisema kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itatekeleza kwa ufanisi Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali katika mwaka huu wa fedha. “Tayari tumeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Mfumo wa Uchumi wa kidijitali nchini. Tanzania inaenda kuwa ya mfano katika upatikanaji wa huduma kwa njia za kidijitali na kuimarisha uchumi wetu” alisema Mhe. Nape.

Mheshimiwa Nape alisema jambo la nne ni kuhakikisha Wizara na Taasisi zake zinatekeleza Dira ya Wizara kuhusu Huduma za Mawasiliano. Dira hiyo ni pamoja na kwanza, kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafika kwenye kila kona ya nchi hii.  Pili, pamoja na kupatikana kwa huduma hizo, amesema lazima huduma hizo ziwe na ubora wa hali ya juu, tatu, ni muhimu pia ziwe salama kwa wananchi wote na waweze kuzitumia bila hofu. Tano, huduma za mawasiliano ziwe za gaharama nafuu na ambazo wananchi wataweza kuzimudu. “na tano, nia yetu ni kuhakikisha huduma zinakuwa na matokeo makubwa kwa watumiaji. Hii ikiwa ni pamoja na kubadilisha maisha yao kwa ujumla kama vile kupata huduma mbalimbali za habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, kufanya malipo kwa kutumia TEHAMA na kadhalika” alifafanua Mhe. Nape.

Hali kadhalika Mheshimiwa Nape alisema jambo la nne kubwa ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma zote zinazotolewa na Serikali na Taasisi zake kwa kutumia namba maalumu ya utambulisho (Jamii Namba) atakayopewa kila mwananchi. “Kila mtanzania awe na namba ya utambulisho  ambayo itakuwa na taarifa zake zote tangu anazaliwa hadi anaondoka duniani. Wizara na Taasisi zake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tunakwenda kuhakikisha kuwa Jamii Namba inaanza kutumika” alisema Mhe. Nape.

Suala la tano alisema ni kuimarisha huduma za Baraza la Ushauri la Watumia Huduma za Mawasiliano. Alisema Baraza hili ni muhimu sana kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini. Alibainisha kuwa kuna laini za simu takribani milioni 61 ambazo zinatumiwa na wananchi kupata huduma mbalimbali na ni muhimu kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano. “Ninawaomba wananchi watoe ushirikiano kwa Baraza hili ili waweze kupata haki zao na kutetewa na Baraza hili ambalo liko kwa ajili yao” alihitimisha Mhe. Nape Nnauye. 

Akizungumza katika hafla ya kufunga Kikao Kazi hicho, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bwana Mohammed Khamis Abdulla amezielekeza Taasisi zote chini ya Wizara ziwe na utaratibu wa kufanya Vikao Kazi (Retreat) kila mwaka mara baada ya kikao cha Viongozi. “Vikao Kazi hivyo viwe ni vya kujipanga jinsi ya kuweka mikakati ya kutekeleza maazimio ya Kikao kazi cha viongozi na pia kujipanga jinsi ya kukabiliana na changamoto za utekelezaji na maboresho ya utendaji kazi wa Taasisi na kuanzimia kwa pamoja utekelezaji wa malengo ya mwaka wa fedha unaofuata” alisema Bwana Mohammed Abdulla.

Kuanzia tarehe 19 hadi 22 Julai 2023, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Taasisi zake (Shirikala Utangazaji Tanzania (TBC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Baraza la Ushauri la Watumiaji huduma za Mawasiliano (TRCA-CCC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Tume ya TEHAMA (ICTC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) na Tume ya Kulinda Taarifa Binafsi. Viongozi Wakuu wa Wizara, Wenyeviti wa Bodi, Wakuu wa Taasisi na Menejimenti zao walihudhuria Kikao kazi hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.