Habari za Punde

Wenye Ulemavu Wanufaika na Program ya Nishati Safi ya Kupikia

 

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Ummy Nderiananga akikabidhi mitungi ya gesi kwa Watu  Wenye Ulemavu katika Wilaya ya Hai wakati wa ziara yake katika Mkoa huo.

Na Mwandishi wetu- Kilimanjaro

Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Ummy Nderiananga ameunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha  watu wenye ulemavu na vikundi vya wanawake kutumia nishati safi ya kupikia kwa kutoa Mitungi ya gesi.

Mhe. Ummy  ametoa mitungi hiyo wakati akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Hai  Mkoani Kilimanjaro huku akisisitiza umuhimu wa nishati hiyo mbadala ambapo amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuhakikisha inapunguza matumizi ya kuni, mkaa ili kulinda afya za wananchi.

Amesema kuwa licha ya athari za kimazingira zinazotokana na ukataji wa miti unaofanywa na Wananchi Matumizi ya nishati chafu yamekuwa na athari zaidi za kiafya.

““Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi katika maeneo mengi  ikiwemo programu ya kumtua mama ndoo kichwani lakini akasema wakina mama wanapata shida wao ndio wapishi sasa ni wakati wa kuwatua kuni kichwani kwa kuwasaidia kupata nishati ya gesi na mimi nimekuja kutekeleza adhma yake ya kumtua mama kuni kichwani” Amesema Mhe.Ummy

Katika hatua nyingine ametoa wito kwa Watu Wenye Ulemavu nchini kutumia fursa ya uanzishwaji wa Vyuo  Vya Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu  ili kupata elimu ya ujuzi  itakayowawezesha kujikwamua kimaisha na kuondokana na hali ya utegemezi.

“Ni muhimu kwa wazazi na walezi wenye  vijana  wenye ulemavu kuwapeleka na kuwaandikisha katika  vyuo vilivyopo Kikanda kupata elimu itakayowajenga kujitegemea kutokana na fani mbalimbali zinazotolewa  ikiwemo Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu (Kanda ya Kaskazini kilichopo mtaa wa Masiwani  Mkoani  Tanga,”Ameeleza.

Awali Akiwasilisha taarifa kuhusu watu wenye ulemavu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bwa. Robert Mwanga alibainisha kwamba Wilaya ya Hai imefanikiwa kuwawezesha watu wenye ulemavu, wanawake na vijana  kiuchumi  kupitia mikopo  ya Halmashauri ambayo ilikuwa inatolewa katika kila Halmashauri Nchi nzima.

“Wanawake, vijana na wenye ulemavu wameboresha mitaji yao na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali na biashara, kupata huduma za kijami kama maji, elimu na afya. Pia tumeendelea kutoa elimu ya fedha, utunzaji wa kumbukumbu kupitia semina ambazo hutolewa na Halmashauri pamoja na kutoa ajira kwa wenye ulemavu 827,”Alieleza Bwa. Mwanga.

Naye Mbunge wa Jimbo la Hai  Mkoani Kilimanjaro Mhe. Saasisha Mafue alipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendela kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu na maji.

“Ipo miradi mingi sana inatekelezwa na Serikali na kwa elimu ni ujenzi wa shule kama  Machame Girls imepokea Milioni 300, Harambee Milioni 487, Ryamungo Milioni 200 miradi ambayo mkandarasi yupo site  yote haya yanafanyika kutokana na nia njema ya Rais wetu,”Alifafanua Mbunge huyo.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Ummy Nderiananga akikabidhi mitungi ya gesi kwa Watu  Wenye Ulemavu katika Wilaya ya Hai wakati wa ziara yake katika Mkoa huo
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Ummy Nderiananga akikabidhi mitungi ya gesi kwa Vikundi vya Wanawake  katika Wilaya ya Hai wakati wa ziara yake mkoani humo
Mbunge wa Jimbo la Hai  Mkoani Kilimanjaro kupitia CCM Mhe. Saasisha Mafue akifafanua jambo katika ziara ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoani humo Mhe. Ummy Nderiananga alipotembelea na kukagua ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT, Wilaya ya Hai.
Baadhi ya watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
Baadhi ya watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Ummy Nderiananga  akikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba ya mtumishi  ikiwa ni muendelezo wa ziara yake  ya kutembelea Wilaya  katika Mkoa wa Kilimanjaro kufuatilia Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Ummy Nderiananga akikabidhi  fimbo nyeupe  kwa wasiyoona  katika Wilaya ya Hai wakati wa ziara yake Mkoani humo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.