Habari za Punde

Balozi wa Marekani apongeza uteuzi wa Dkt. Biteko. Dkt. Biteko aahidi ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa Sekta ya Nishati.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko (kulia) akizungumza na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle, katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati Jijini Dar es Salaam leo, Septemba 13, 2023. 
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle (kushoto) akimweleza jambo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati Jijini Dar es Salaam leo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko (kulia) akiwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati Jijini Dar es Salaam leo, Septemba 13, 2023. 


Na Janeth Mesomapya

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle, alipomtembelea leo, Septemba 13, 2023 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.

 

Dkt. Battle amemtembelea Mhe. Biteko kwa lengo la kumpongeza kwa uteuzi na majukumu yake mapya ikiwa ni pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kisekta baina ya nchi hizo mbili.

 

Katika mazungumzo yao Mhe. Biteko ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati ikiwemo ya uzalishaji umeme pamoja na Mradi wa kubadili Gesi Asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG).

 

Mhe. Biteko amesema kuwa, majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji wa Mradi wa LNG yako katika hatua nzuri na wataalamu wanaendelea kupitia vipengele vya mkataba huo ili kuhakikisha kila upande umeridhika. 

 

Aidha amegusia kuwa upo uwezekano wa kurudia baadhi ya vipengele ili kuviboresha zaidi. 

 

“Tunaendelea kupitia na kuboresha baadhi ya vipengele vya mkataba huu ili pindi utakapokuwa tayari uwe nyenzo ya kuhakikisha matarajio na manufaa ya mradi huu yanafikiwa,” alifafanua Mhe. Biteko.

 

Naye Balozi Battle alimtaarifu Mhe. Biteko kuwa zipo kampuni mbili za Kimarekani Astra Energy na Upepo Energy zenye lengo la kuwekeza nchini Tanzania kwenye eneo la uzalishaji umeme na tayari zimekwishawasilisha rasmi nia yao ya kuwekeza hapa nchini.

 

Akizungumzia kuhusu suala hilo Mhe. Biteko ameahidi kufuatilia kuhusu wawekezaji hao kutokana na uhitaji mkubwa wa Nishati ya Umeme hapa nchini kwa sasa.

 

Vivyo hivyo Balozi Battle ameeleza kuwa ana imani Mhe. Biteko atafanya vizuri katika kusimamia Sekta ya Nishati ikizingatiwa kuwa ana uzoefu mkubwa katika Sekta ya Uziduaji ikiwa ni pamoja na uzoefu wa aina ya mikataba aliyokutana nayo kipindi akiwa Waziri wa Madini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.