WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya ziara na kusilikiliza kero za wananchi, haoni ni kwa nini watumishi wengine wa umma wanashindwa kufanya hivyo.
“Iwapo Mkuu wa nchi, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anaenda kote nchini na kusikiliza wananchi, je ninyi ni akina nani? Nilishasema mtenge siku tatu katika wiki mwende vijijini na kuwasikiliza wananchi,” alisema.
Ameyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Septemba 21, 2023) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nguruka, wilayani humo.
“Mheshimiwa DC simamia watu wako waende vijijini. Nilishasema hata kama magari ni machache, pangeni ratiba, mbebane na mwende kuwasikiliza wananchi. Gari litawapeleka na kuwaacha kwenye vijiji husika na wakati linarudi litawapitia wote. Nenda mkawasikilize wananchi, nenda mkawatumikie wananchi,” alisisitiza.
Alisema Uvinza ni miongoni mwa Halmashauri za Wilaya 15 zilizoanzishwa ili kusogeza huduma kwa wananchi na akawataka viongozi wa wilaya hiyo wajipange kupima viwanja na kutoa hati kwa wananchi wao. “Mheshimiwa Rais ameagiza viwanja vipimwe na watu wapatiwe hati ili waweze kukopa Benki na kuongeza mitaji yao.”
Aliitaka Halmashauri ya Uvinza ijipange kwa kupima viwanja vya wananchi ili baadaye wasilazimike kuwaambia wabomoe kwa kuwa wamejenga kwenye maeneo yaliyopangiwa matumizi mengine.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, SEPTEMBA 22, 2023.
No comments:
Post a Comment