Habari za Punde

Tanzania na Norway Zasaini Makubaliano Kukabili Mabadiliko ya Tabianchi

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim wakisaini makubaliano ya ushirikiani kati ya Serikali ya Tanzania na Norway kuhusu ushirikiano katika hifadhi ya mazingira jijini Dar es Salaam leo Septemba 07, 2023. Aneyeshuhudia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo.


Serikali ya Tanzania imenufaika na shilingi bilioni 7.3 kutoka Serikali ya Norway kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na inayotekelezwa nchini.

Hayo yamejiri baada ya Serikali hizo mbili kusaini Makubaliano ya kushirikiana katika shughuli za mazingira, hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 07, 2023.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania itajengewa uwezo katika utekelezaji wa shughuli za mazingira.

Alisema makubaliano hayo ni chachu katika kuijengea Tanzania kuweza kunuifaika na fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutoka nchi zilizoendelea ambazo ziliahidi.

Pia, alisema Norway imeiunga mkono Tanzania katika mikakati yake ikiwemo kupunguza gesi joto, utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032 pamoja Sera ya Uchumi wa Bluu.   

“Makubaliano tuliyosaini leo yatasaidia katika miradi yetu ya kimazingira katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji, afya na ardhi na tuishukuru sana Serikali ya Norway, na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tunafurahi sana kwa miradi hii ambayo inakwenda kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dkt. Jafo.

Kwa upande wake Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim aliyesaini kwa niaba ya Serikali ya Norway alisema kuwa makubaliano hayo ni matunda ya uhusiano wa muda mrefu wa Serikali hizo mbili.

Alisema nchi yake imejipanga katika kuyatendea haki makubaliano hayo kwa kuelekeza miradi hiyo kwa wananchi wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yao.

Mhe. Anne alisema kuwa Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kufanya utafiti kwa ajili ya katika kuimarisha usimamizi wa Biashara ya Kaboni ambayo imeshika kasi hapa nchini.

Naye Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Maendeleo (UNFCC) Bw. Peter Malika alisema fedha hizo zilizotolewa zitasambazwa katika wilaya sita za Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kusaidai katika miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema pia kutakuwa na mafunzo kwa jamii zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi kuhusu namna ya kutambua changamoto hizo kwa ajili ya mikakati ya kuanzisha miradi.

Aprili 21, 2008 nchi hizo mbili zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi hatua iliyoanzisha Kituo cha Taifa Kufuatilia Kaboni (NCMC).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim wakionesha nyaraka za makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Norway kuhusu ushirikiano katika hifadhi ya mazingira jijini Dar es Salaam leo Septemba 07, 2023. 

Balozi wa Norway nchini Tanzania na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Maendeleo (UNFCC) Bw. Peter Malika wakisaini makubaliano ya kushirikiana ya kiasi cha shilingi bilioni 7.3 kwa ajili ya kusaidia katika wilaya za Mkoa wa Dodoma katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Norway kuhusu ushirikiano katika hifadhi ya mazingira jijini Dar es Salaam leo Septemba 07, 2023. Kushoto ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Norway kuhusu ushirikiano katika hifadhi ya mazingira jijini Dar es Salaam leo Septemba 07, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.