Meneja utekelezaji wa mradi wa Viungo Ali Said Juma akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa wa kamati za Wilaya za mradi wa viungo juu ya ukusanyaji wa takwimu na ustadi wa kuandika ripoti huko Ofisi za viungo Mwanakwerekwe Zanzibar
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO
Na fauzia Mussa, Maelezo
WADAU wa maendeleo wamesisitiza kutolewa kwa elimu ya uandishi wa ripoti ili kuona ripoti zinazoandaliwa zinakwenda sambamba na utekelezaji wa miradi inayoendeshwa kwa kuonesha thamani halisi ya fedha zinazotumika.
Akifungua mafunzo kwa maofisa wa kamati za Wilaya za mradi wa viungo Ofisa mkuu wa mawasiliano wa mradi huo Saphia Ngalapi alisema ripoti nyingi zinazoandaliwa zinakuwa na mapungufu hasa ya kuonesha thamani ya fedha zilizotumika katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Alisema Taasisi za Serikali na Binafsi zimekuwa zikitekeleza miradi mbalimbali inayotokana na matokeo ya ripoti ,hivyo ipo haja ya ripoti hizo kuzingatia mahitaji muhimu ili wafuatiliaji waweze kuzitumia kwa ufanisi na weledi.
“ ripoti hukusanya taarifa muhimu ambazo hutumika katika shughuli mbalimbali ,hivyo bila ya kuwa na taarifa sahihi hatuwezi kufikia malengo.”
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka washiriki hao kwenda kuyafanyia kazi mafunzo hayo sambamba na kuwa mabalozi wazuri wa kwenda kuwafundisha wenzao ili kuona taaluma hiyo inaleta tija kwao na taifa kwa ujumla.
Akiwasilisha mada ya ukusanyaji wa takwimu na kuandika ripoti Ofisa ufuatiliaji na tathmini Malik Rashid alisema datazinapokusanywa husaidia kutumika katika kuandika ripoti kwa ukamilifu na kuwasaidia watumiaji kujua maeneo muhimu ya kuanza kuyafanyia kazi.
Hivyo amewasisitiza maofisa hao kuzingatia mambo muhimu katika kuandaa ripoti ikiwemo ubora na takwimu zenye taarifa sahihi,
Nae meneja utekelezaji mradi wa viungo Ali Saidi Juma alisema lengo la mradi huo ni kuwaleta pamoja wadau wa kilimo cha mbogamboga na matunda pamoja na kuongeza thamani bidhaa hizo ili kuongeza kipato cha wakulima wadogo wadogo.
Nao washiriki wa mafunzo hayo walishukuru kupatiwa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kuongeza uwezo na uwelewa wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mradi wa viungo unatekelezwa kwa mashirikiano na taasisi tatu ikiwemo PDF,community, forest pemba (CFP) pamoja na Tamwa Zanzibar chini ya ufadhili wa umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya kilimo.
No comments:
Post a Comment