Habari za Punde

Wakandarasi watakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa masoko



 Wakandarasi na washauri elekezi katika ujenzi wa mradi wa masoko ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini wametakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa masoko hayo na kuhakikisha yanamalizika kwa wakati uliopangwa ili yaweze kufunguliwa katika sherehe za Mapinduzi mapema Mwezi Januari 2024.

 

Akikagua muendelezo wa ujenzi wa masoko hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema licha ya jitihada zinazochukuliwa na wakandarasi na washauri elekezi katika ujenzi huo bado wana wajibu wa kuongeza kasi na juhudi zaidi kuhakikisha mradi huo unamalizika kwa muda uliopangwa na kwa viwango vya juu.

 

Aidha amewataka wakandarasi wa ujenzi wa masoko hayo kujenga kwa kutumia vifaa vyenye ubora na kuwapongeza kwa kukataa kupokea Vifaa visivyo na viwango ili kujenga majengo yaliyo imara zaidi na yatakayodumu kwa muda mrefu.

 

 

Amesema maono ya Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussen Ali Mwinyi ya kuona ipo haja ya kujengwa masoko makubwa na ya kisasa visiwani hapa yatakayokidhi mahitaji ya wafanyabishara yatatatua changamoto za wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanya biashara zao katika maeneo yasiyo rasmi.

 

 

Mhe. Hemed amewataka wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara zao katika masoko hayo na wale wapya wajiandae kisaikolojia kufanya kazi kwa uweledi na umakini katika masoko hayo mapya kwani hawataruhusiwa kufanya biashara pembeni mwa barabara na maeneo yasiyo rasmi jambo ambalo litasaidia kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali na kutunza usafi katika masoko hayo.

 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza Wakurugenzi wa manispaa kuhakikisha wanatoa elimu na maelekezo kwa wafanyabiashara juu ya namna bora watakavyoyatumia masoko hayo  

 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara maalum za SMZ Mhe. Massoud Ali Moh'd amesema ziara hiyo ya  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inaamsha ari na hamasa ya kufanya kazi muda wote tena kwa ustadi wa hali ya juu.

 

Ameeleza kuwa Makamu wa  Pili wa Rais wa Zanzibar amekuwa akisahuri na kutoa miongozo inachangia kuharakisha umalizikaji wa ujenzi wa mradi wa masoko hayo.

 

Nae Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Khamis Bakar Khamis ambae ni Mkandarasi wa    Soko la Jumbi amesema watahakikisha wanafanya kazi kwa muda wote ili ujenzi huo  umalizike kwa wakati na kwa mafanikio makubwa.

 

Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo katika ujenzi huo watahakikisha ifikapo mwezi Disemba mwaka huu masoko hayo yamemalizika na kukabidhiwa Serikalini.  

 

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Serikali ya Mkoa imekuwa ikifuatilia kila hatua ya ujenzi wa masoko hayo lengo ni kuhakikisha yanajengwa kwa viwango vya hali ya juu na kumalizika kwa wakati ili kuweza kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wananchi kutumia masoko hayo.

 

Mhanidisi Ali Hilal Mohd ambae ni Mshauri elekezi katika ujenzi wa mradi wa masoko hayo kutoka wakala wa usimamizi wa majengo (ZBS) amesema watahakikisha wanasimamia vyema ujenzi huo ili uweze kukamilika ukiwa na ubora na viwango vya juu kama walivyokubaliana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

 

………………….

Luluwa Ali

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

14/09/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.