SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar imesema Utalii ni kipaombele chake cha kwanza kwenye mnyororo wa
sekta za Uchumi wa Buluu kutokana na kuchangia asilimia 30 ya pato la taifa
mbali ya sekta nyengine za maendeleo.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo Ikulu,
Zanzibar alipozungumza na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza, Tony Blair
aliefika na ujumbe wake.
Dk. Mwinyi alimueleza
mgeni wake huyo kwamba, Zanzibar ina utalii wa asili wa fukwe na urithi lakini
kwa sasa inahitaji kwenda mbali kuboresha utalii wake kwa kuangalia zaidi
utalii wa mikutano na michezo.
Rais Dk. Mwinyi amezitaja
sekta nyengine za Uchumi wa Buluu ni pamoja na Bandari ambayo inamchango mkubwa
wa uchumi wa Zanzibar na ina mahitaji ya uwekezaji kwenye eneo hilo hasa
bandari jumuishi itakayotoa huduma zote ikiwemo kuruhusu meli kubwa kushusha na
kupakia mizigo mingi ya vyakula, nafaka, mafuta na mahitaji mengine ya uchumi.
Akizungumzia Sekta ya
usafirishaji kwenye Uchumi wa Buluu, Rais Dk. Mwinyi alisema kwa vile Zanzibar
imezungukwa na bahari sekta hiyo pia ni muhimu kwa uchumi wake hiyo inahitaji
uwekezaji mkubwa ili kuuimarisha usafiri wa majini kwa abiria na mizigo.
Kuhusu sekta ya Mafuta
na gesi, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri Mkuu huyo wa Zamani wa Uingereza
kwamba Zanzibar inahitaji uwekezaji mkubwa ili kuimarisha sekta ya biashara na
uchumi kupitia bandari.
Pia, Rais Dk. Mwinyi
alieleza, ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
taasisi ya Tony Blair hasa kwenye miradi mbalimbali ya huduma za jamii iliwemo
elimu na afya.
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza alisifia uzuri kisiwa cha Zanzibar
ulivyobarikiwa kuwa na haiba na mwambao mzuri wa kumvutia kila mgeni aingiae na
kuongeza kuwa Zanzibar imejijengea sifa duniani ya kuwa na vivutia vizuri vya
utalii.
Aidha, aliishauri
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza mvuto zaidi kwa kuendelea kukipatia
sifa nzuri kisiwa cha Pemba kwani ni bahati kubwa kwa Zanzibar kuwa na kisiwa
kizuri kama hicho ambacho ni mfano mzuri wa kivutio cha utalii duniani.
Hivyo, aliishauri
Serikali kuendelea kudumisha vivutio vyake vya utalii na kuendelea kuiongezea
sifa Zanzibar kiutalii duniani kote.
Tony Blair ni mwanasiasa
mkongwe nchini Uingereza aliehudumu nafasi ya Uwaziri mkuu kutoka mwaka 1997
hadi mwaka 2007 anakua Waziri Mkuu wa pili kuongoza nafasi hiyo kwa muda mrefu
Uingereza baada ya Magret Thatcher aliehudumu nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka
11. Blair pia ni Mwenyekiti wa taasisi ta Tony Blair (TBI).
No comments:
Post a Comment