RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amevinasihi vikosi
vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza uadilifu na uwajibikaji wa
majukumu yao ya kila siku.
Dk. Mwinyi
ambae ni Kamanda Mkuu wa Idara Maalum ya vikosi vya SMZ,
alitoa nasaha hizo viwanja vya JKU – Kama, alipozungmuza na wapiganaji kwa
lengo la kuwapongeza kutokana na juhudi zao za kuhakikisha amani na utulivu nchini
vinaendelea kuimarishwa.
Alivitaka vikosi
hivyo kuweka mbele maslahi ya nchi kwanza, uwajibikaji pamoja na kusimamia
uadilifu jeshini.
Rais Dk.
Mwinyi alivisisitiza vikosi hivyo juu ya suala zima la kusimamia nidhamu kwenye
maeneo yao ya kazi ili kufanya kazi zao kwa uadilifu.
“Jeshi ni
nidhamu ikikosekana nidhamu katika jeshi basi hapo hakuna jeshi” alikazia Rais
Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi
pia, alivipongeza vikosi hivyo kwa jitihada zao za kutoa huduma bora kwa jamii
wakiwemo Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kupitia hospitali yao iliopo Bububu
pamoja na hospitali ya JKU, Saateni kwa huduma za afya wanazozitoa kwa wananchi
na nyengine za jamii vikiwemo vyuo vya amali na taaluma.
Alivitaka
vikosi hivyo kuwa mfano mzuri wa kutoa huduma bora kwa raia hasa kwenye vituo
vyao vya afya na taaluma vinavyohudumia jamii.
Halikadhalika,
Rais Dk. Mwinyi aliwaagiza wakuu wa vikosi hivyo kuendelea kusimamia uwajibikaji
ili kuwe na tofauti baina ya hospitali za jeshi na za raia ili wananchi wapate
huduma bora.
Pia, Dk. Mwinyi alivieleza vikosi hivyo
kuwa vinajukumu la kutoa malezi bora kwa vijana na kuhakisha wanatoa vijana wazalendo
wenye uchungu wa nchi yao watakaopigania maslahi ya taifa lao.
Akizungumzia suala
la kuwajengea uwezo maofisa na wapiganaji wa vikosi hivyo, Rais Dk. Mwinyi
aliwataka wakuu wa vikosi hivyo kuwaongezea uwezo wa kitaaluma maofisa hao kwa kuwapatia
fursa za mafuzo.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo, Waziri wa Idara Maalum ya vikosi vya SMZ, Masoud Ali
Muhammed alisema, Idara Maalum ya vikosi vya SMZ zote
tano zikotayari kuendeleza jukumu mama la kuimarisha na kuendeleza amani,
utulivu na mshikamano uliopo nchini vinaendelea kusimama wakati taifa likiendeleza
maendeleo ya watu wake.
Alisema, Idara
hizo pia zitaendelea kutekeleza maagizo, maono, mipango na fikra za Kamanda
Mkuu kwa utii wa hali ya juu.
Akiwasilisha risala
ya vikosi vitano vya Idara Maalum ya SMZ, Katibu Mkuu wa Idara hiyo, Issa
Mahafoudh Haji alisifu juhudi kubwa ya Kamanda Mkuu wa Idara Maalum ya vikosi
vya SMZ, Rais Dk. Mwinyi aliyoifanya kwa vikosi hivyo.
Alimshukuru
Rais Dk. Mwinyi kwa kuvishirikisha vikosi hivyo kwenye ujenzi wa miradi mikubwa
ya maendeleo nchini na kueleza kuwa imewaongezea uwezo na nguvu za kiuchumi kwa
kutatua baadhi ya changamoto zao.
Pia, alieleza
ushiriki wao kwenye miradi hiyo, umetanua uwezo wao wa ufahamu na ujuzi wa
kutekeleza majukumu yao ya kila siku pamoja na kusifu hatua ya kuwapandishia
mishahara makamanda na wapiganaji kufuatia nyongeza ya mishahara aliyoitoa kwa watumishi
wa umma wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vikosi vya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vinaundwa na Jeshi la kujenga Uchumi (JKU), (KMKM),
Vikosi vya Uokozi na Zimamoto, Valantia (KVZ) na Chuo cha Mafunzo.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment