Habari za Punde

Uzinduzi wa Mashindano ya Kuhifadhi Qur-an Afrika Mashariki

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na waumini wa dini ya kiislam wakati akizindua mashindano ya kuhifadhi Qur-an Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika machi 30 mwaka huu katika viwanja vya Amani Complex  hafla iliyofanyika Madinatu Al bahr Mbweni Zanzibar.

Na Rahma Khamis Maelezo.

Makamu wa Pili wa Rais Alhaj Hemed Suleiman Abdullah amewataka wazazi na walezi kuwahimiza vijana na jamii kwa ujumla kuzidi kushikamana na Qur-an kwa kuisoma,kuihifadhi na kufuata maamrisho na makatazo yake kwani ndio muongozo kwa wanadamu wote.


Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Madinat-Albahr Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akizindua  mashindano ya kuhifadhi Qur-an Afrika Mashariki.


Amesema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono harakati hizo ambazo dhamira yake ni kuisaidia jamii katika kuendeleza dini ya kiislamu na kuimarisha maadili mema ambayo ni nguzo kwa jamii inayoendele  kudumisha amani na umoja uliopo Nchini.


Alhajj Hemed  ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua kazi kubwa zinazofanywa na Ofisi ya Mufti Mkuu na Shirika la Utangazaji Zanzibar  katika kujenga jamii yenye maadili mema,hivyo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kuona Zanzibar inazalisha vijana wenye kufaata maadili .


"Tunapozungumza Qur-an huwa tunazungumzia maisha ya dunia na na Akhera tunakokwenda  hivyo hatuna budi kuisoma na kuihifadhi ili tupate maisha bora zaidi" Alhaj Hemed alisisitiza.

 

"Ni dhahiri kuwa endapo vijana wetu hatutawawekea misingi imara ya kitabia na kuifahamu dini yao ,watakua rahisi kufuata tamaduni za kigeni ambazo zinakwenda kinyume na mila ,Silla na desturi zetu " alifafanua Makamu wa Pili.


Akitoa maelezo mafupi Katibu Mtendaji Ofisi Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume amefahamisha kuwa mwenye kushika Qur-an Mwenyezi Mungu humuinua hivyo ipo haja kwa waislamu kujitahidi kuisoma na kuhifadhi ili kupata radhi za Allah SW.


Kwa upande Mkurugenzi wa ZBC Ramadhan Bukini  amesema kuwa lengo  la kuanzisha mashindano hayo ni kuitangaza Qur-an kwani upo umuhimu wa kufanya hivyo kutokana na  mwezi wa ramadhani ndipo iliposhushwa Qur-an hiyo.


Mapema alifahamisha kuwa mashindano hayo  yatafanyika machi 30 mwezi huu katika Uwanja wa Amani Complex na kuwataka wananchi kujitokeza kuhudhuria kwa wingi ili kupata radhi za Allah.


Mkurugenzi Bukini ameeleza kuwa awali  walikua wakifanya mashindano hayo ndani ya Zanzibar  kwa njia ya  Tartili lakini kwa mwaka huu wameimarisha zaidi kwa kushirikisha nchi za Afrika Mashariki  ikiwemo Kenya Comoro, Burundi ,Uganda na Wenyeji Tanzania.


Mashindano hayo yameandaliwa na Shirika la Utangazaji ZBC kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu Qur-an ni nguzo ya kutuunganisha”.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ,Katiba , Sheria Utumishi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Mhe Hemed Suleiman Abdulla kuzindua mashindano ya kuhifadhi Qur -an Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika machi 30 mwaka huu katika viwanja vya Amani Complex  hafla iliyofanyika madinatu Al bahr Mbweni Zanzibar.
Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu wakifuatilia uzinduzi wa mashindano ya kuhifadhi Qur -an Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika machi 30 mwaka huu katika viwanja vya Amani Complex hafla iliyofanyika madinatu Al bahr mbweni Zanzibar.Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu wakifuatilia uzinduzi wa mashindano ya kuhifadhi Qur -an Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika machi 30 mwaka huu katika viwanja vya Amani Complex hafla iliyofanyika madinatu Al bahr mbweni Zanzibar.

Picha na Fauzia Mussa --Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.