RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa India Nchini Tanzania Mhe.Bishwadip Dey, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 20-8-2024, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema miongoni mwa mafanikio makubwa inayojivunia kutokana na ushirikiano wa diplomasia uliopo baina yake na Serikali ya India ni kuanzishwa kwa tawi la Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT Madras, Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi
wa India nchini, Mhe. Shri Bishwadip Dey aliyefika
kujitambulisha.
Amesema, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT Madras ni
fursa muhimu kwa sekta ya elimu Zanzibar itakayoleta mageuzi makubwa ya mifumo na
kukuza teknolojia nchini.
Dk. Mwinyi alimuhakikishia Balozi huyo ushirikiano mzuri uliopo
baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na chuo hicho kwa kushirikiana na
Serikali ya India ni jitihada zao za kuimarisha uhusiano wa Diplomasia baina
yao.
Amesema, India imekua mdau mkubwa kwa maendeleo ya
Zanzibar kupitia sekta mbalimbali ikiwemo miradi mikubwa ya maji safi na
salama, sekta ya afya na elimu ambapo imekua ikishirikiana kwa miaka mingi.
Hivyo, ameiomba India kupitia teknolojia kubwa waliyonayo
na kwa uweledi wa mitandao ya kijamii iliyobobea kuendelea kuitangaza Zanzibar
Kimataifa kupitia tawi la Chuo hicho duniani pamoja na sekta za biashara na uwekezaji.
Dk. Mwinyi alisema, sekta za Afya na Elimu zimepata
ushirikiano mzuri kutoka India kwa kuendelea kuwapokea Watanzania wengi kwa
matibabu nchini humo sambamba na Watanzania wanaoendeleza masomo yao pamoja na
ushirikiano wa biashara uliopo baina ya pande mbili za ushirikiano.
Akizungumzia sekta ya Utalii ikiwa ni sekta kiongozi ya
Uchumi wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alimueleza balozi huyo kuangalia uwezekano
wa kuongeza watalii wengi wa India, alimueleza balozi huyo kwamba watalii wengi
wanaoingia Zanzbar ni kutoka Ulaya mashariki na kwengineko duniani.
Naye, Balozi Shri Bishwadip alimuhakikishia Rais Dk.
Mwinyi kuendeleza historia ya ushirikiano uliopo wa pande mbili hizo hasa
kwenye kuboresha sekta za biashara, Uchumi, utalii na uwekezaji pia alimuahidi
Rais Dk. Mwinyi kuendelea kupokea wafanyabiashara wakubwa kutoka India, wenye
nia ya kuwekeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Chuo cha IIT Madsa kilianzishwa Zanzibar, mwezi Oktoba
mwaka jana kwa ushiriano wa Serikali ya SMZ na Serikali ya India ambacho kinatarajiwa
kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu, Zanzibar hasa kutoa fursa kwa
wazawa ya kujifunza teknolojia.
Uhusiano wa diplomasia baina ya Tanzania na India ni wa
historia ambapo India ilifungua Ubalozi wake Dar es Salaam mwezi Novemba mwaka
1962 na mwaka 1974 ikafungua ubalozi mdogo Zanzibar. Uhusiano wa pande mbili
hizo umeendelea kuimarika kwa fursa nyingi za biashara na maendeleo kupatikana.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa India Nchini Tanzania Mhe.Bishwadip Dey, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 20-8-2024, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment