SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inajipanga kujenga uwanja mkubwa wa michezo utakaokuwa na vigezo vinavyokubalika na Shirikisho la Soka Duniani FIFA pamoja na Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo
Ikulu, Zanzibar alipokutana na viongozi na wachezaji wa Klabu ya Simba ya Dar
es Salaam waliofika kumsalimia kabla ya mchezo wao wa kesho dhidi ya Azam
utakaochezwa Uwanja wa Amani Complex, majira ya saa mbili usiku.
Alisema, lengo la Serikali ni kuhakikisha michuano ya soka inayowashirikisha wachezaji
wanaocheza ligi za ndani (Chan) na ile ya michuano ya soka ya mataifa ya Afrika
kwa timu za taifa (AFCON), kuwa Zanzibar ni sehemu itakayochezwa michezo hiyo.
Amesema, Zanzibar imefanikiwa kwenye maeneo
mbalimbali ya utalii ikiwemo utalii wa fukwe, urithi na makumbusho, hivyo
wakati umefika sasa kwa Serikali na wadau wa utalii, kuangalia maeneo mengine
ya kuutangaza utalii ikiwemo michezo.
Halikadhalika, alisema Serikali inaendelea kuwekeza na
kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kuendeleza ujenzi wa viwanja vya michezo
vyenye hadhi ya kimataifa kwa maeneo yote ili michuano mikubwa ichezwe
Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameelezea dhamira ya Simba ya
kujenga kituo cha kuwaendeleza vijana katika mchezo wa soka hapa Zanzibar
(soccer academy) kuwa ni jambo jema na kuwaahidi Serikali ipo tayari kuwaunga
mkono kwa kuwapa eneo la ujenzi wa kituo hicho.
Pia, amevitaka vilabu vya michezo nchini kucheza
michezo yao mingi Zanzibar ili kuimarisha sekta ya michezo pamoja kuinua mwamko
wa vijana kupenda michezo.
Rais, Dk. Mwinyi amebainisha kuwa Zanzibar ina
vipaji vingi vya vijana wanaohitaji kuendelezwa hususan kwenye mchezo wa soka
ili kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuzisaidia timu zao na timu za
taifa.
Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu
amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Klabu hiyo ipo tayari kuitangaza
Zanzibar kimataifa kupitia utalii wa michezo.
Vilevile, amepongeza juhudi za Rais Mwinyi
kuendeleza viwanja vya michezo kila wilaya Unguja na Pemba, kwani michezo ni
nyezo muhimu ya kukuza umoja, furaha na upendo miongoni mwa wananchi.
Simba Sports Club hivi karibuni ilifanikiwa kuingia
hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuitoa
timu ya “Ahly Tripol” ya Libya na kuingia hatua ya makundi kwa mara ya saba.
IDARA YA
MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment