Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka wadau mbali
mbali katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kurithisha Zanzibar kuwa ya Kijani
kuhakikisha wanazianisha na kuzikabili
ipasavyo changamoto zinazojitokeza hasa katika upatikanaji wa miche ya miti
mbali mbali ili kuufanya Mradi huo kutekelezeka kwa ufanisi na kutimiza malengo
yaliyowekwa na serikali.
Mhe. Othman
ameyasema hayo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokutana na wadau mbali
mbali wa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kuirejesha Zanzibar kuwa ya kijani
kufanya tathmini ya ziara yake ya kimazingira katika maeneo mbali ya visiwa vya
Unguja na Pemba hivi karibuni.
Mhe. Makamu
amefahamisha kwamba maeneo mbali mbali aliyoyatembelea katika ziara hiyo
hayajatumika ipasavyo katika kuatika kiwango toshelevu cha miche ya miti ya
matunda ya aina mbali mbali jambo
linalohitaji kufanyiwa kazi kuelekea utekelezaji wa mpango huo ili kuleta
ufanisi.
Amesema
kwamba kuna haja kubwa kwa wadau hao kuhakikisha masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa
mpango huo ukiwemo mfumo wa utekelezaji kuyawekea utaratibu rasmi mapema na
kutoa hakikisho katika utapatikanaji wa mahitaji ikiwemo miche, rasilimali na
mahitaji mengine muhimu na kuwashirikisha makundi yote ya watu jambo litakalosaidia kubadili tabia za jamii
katika kupenda miti kwa kuhakikisha kwamba wanashiriki katika kupanda na
kuitunza.
Mhe. Othman
amefahamisha kwamba ni lazima wadau hao
kutambua kwamba mpango huo utekelezaji wake kiufanisi unahitaji ushiriki sahihi
wa kila kundi ndani ya jamii kwa kuhakikisha watu wote wakubwa wa wadogo wanajengewa
utamaduni mpya endelevu wa kushiriki kupanda miti na kuipenda jambo litakaloiwezesha
Zanzibar kurudi kuwa ya kijani.
Amesema
kwamba nilazima wadau wote kuisisitiza jamii kwamba ushirikishwaji wa makundi
yote kadri inavyowezekana ni sehemu muhimu katika kuleta ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo
ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira ya kuwavutia watu waweze kushiriki
vyema kwenye utekelezaji wa mpango huo muhimu.
Aidha Mhe.
Othman amewakumbusha wadau hao kuhakikisha kwamba wanayainisha maeneo yote
yanayohitaji kuendelezwa yakiwemo maeneo yanayomilikiwa na wawekezaji ambayo
yanaweza kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuwashirikisha wawekezaji
wenyewe jambo litakaloleta ufanisi zaidi.
Mhe. Othman
amesema kwamba kwamba wale wadau ambao tayari wameanzisha sauala la upandaji
miti kwenye mradi huo ni vyema kusajiliwa ili kutambuliwa katika kuongeza
ushiriki wao pamoja na kufanyiwa tathimini katika viwango mbali mbali vya
utekelezaji.
Aliwataka
wadau kwamba kutambua hali ya kimazingira Zanzibar ni mbaya hasa kwa vile
misitu mingi nahata iliyohifadhiwa imevamiwa kwa kukatwa ukiwemo hata ujenzi wa
makaazi na baadhi kuwa na vijiji hivyo ni vyema kujipanga kwa juhudi za pamoja kwa kuwa ndio njia pekee itakayosaidia
kuirejesha Zanzibar katika hali ya mazingira bora ya kijani.
Kwa upande
wake katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maryam Juma Sadalla amewashukuru wadau hao kwa kuunga
mkono agizo la serikali katika utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kuirejesha
Zanzibar kuwa ya kijani na kusisitiza kwamba ushirikiano uendelee zaidi katika
kufanikisha suala hilo.
Nao wadau
waliohudhuria katika kikao hicho wameleza kwamba kuna umuhimu wa kujipanga
vyema katika kufanikisha utekelezaji wa suala hilo ikiwa ni pamoja na kuona
changamoto za kupanda miti na kuitunza kwa kuishirikisha vyema jamiii hasa
kwenye maeneo ambayo yameharibiwa ili kuweza kuyadhibiti kwa kupandwa upya miti
ya misitu.
Wamesema
kwamba baadhi ya Wilaya na Mansispaa tayari wameanza utekelezaji wa
utayarishaji wa bustani na upandaji wa miti ya aina mbali mbali hivyo kuwepo
mradi huo ni kuongeza nguvu na kasi ya kupandwa miti katika maeneo mbali mbali
ya Zanzibar.
Hata hivyo,
wametaka serikali kuhakikisha kwamba serikali inavyanya juhudi zaidi ya kutoa
elimu kwa jamii ili kujenga mwamko zaidi
ikiwa ni pamoja na kutengeneza fursa mbadala kwa vijana
wanaojishirikisha na kazi za uharibifu wa mazingira kwa uchimbaji wa mchanga
holela katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Kikao hicho
kimewashirikisha baadhi ya makatibu wakuu wakurugenzi wa mabaraza ya miji na
Halimashauri pamoja na maafisa mbali mbali wanaohusika na masuala ya Mazingira
na maliasili ikiwemo misitu na za aina mbali mbali Zanzibar.
Imetolewa
na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha
Habari leo Jumatatu tarehe 07.10.2024.
No comments:
Post a Comment