Mwandishi Wetu.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye
mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa ambapo zoezi
hilo litafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 12 hadi 18
Januari, 2025.
Hayo yameanishwa kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe.
Jacobs Mwambegele iliyosomwa kwa niaba yake kwenye
mikutano ya Tume na wadau wa uchaguzi iliyofanyika leo
tarehe 31 Desemba, 2024 kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe,
Songwe na Rukwa.
Mhe. Mwambegele ambaye aliwakilishwa na wakurugenzi
mbalimbali wa Tume kwenye mikutano hiyo, amesema mikoa
hiyo itafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa tisa na
kwamba tayari Tume imekamilisha uboreshaji kwenye mikoa
19 ambayo ilijumuisha mizunguko nane kati ya mizunguko 13
ambayo imepangwa kukabilisha zoezi hilo nchini.
“Leo tupo hapa Songwe na wenzetu wapo kwenye mikoa ya
Njombe, Rukwa na Ruvuma ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji
wa Daftari kwenye mkoa huu wa Songwe, Njombe, Rukwa na
mkoani Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa,
Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya
Songea, zoezi litakalofanyika kwa muda wa siku saba kuanzia
tarehe 12 Januari, 2025 na kukamilika tarehe 18 Januari,
2025 na ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa
2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” imesema sehemu
ya hotuba hiyo.
Ameitaja mikoa ambayo tayari imekamisha zoezi hilo kuwa ni
Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga,
Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida.
“Mikoa mingine ni mikoa ya Zanzibar ambayo ni Mjini
Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba,
Kaskazini Pemba, Arusha na Kilimanjaro. Kwa sasa mikoa
miwili ya Mbeya na Iringa inatarajia kukamilisha zoezi hilo
tarehe 02 Januari, 2025,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.
Mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani
iliyowasilishwa kwa niaba yake kwenye mikutano hiyo
imeanisha kwamba kwenye mikoa hiyo jumla ya wapiga kura
wapya 475,743 wanatarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura.
Mada hiyo imeanisha kuwa uboreshaji wa Daftari
utakapokamilika, mikoa hiyo inatarajiwa kuwa na jumla ya
wapiga kura 3,091,485 ikilinganishwa na idadi ya wapiga
kura 2,615,742 waliokuwemo kwenye Daftari mwaka 2020.
“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo
watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa
wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20,
lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza
kujiandikisha,” imesema sehemu ya mada hiyo.
Mada hiyo imeanishwa kuwa kutakuwa na vituo 3,785 ikiwa
ni ongezeko la vituo 233 kutoka vituo 3,552 vilivyokuwepo
mwaka 2020.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment