Habari za Punde

Serikali Imefanya Uwekezaji Mkubwa kwa TMA - MAJALIWA * Lengo ni Kuwezesha Utoaji wa Utabiri na Tahadhari za Hali Mbaya ya Hewa

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe ili kuruhusu puto lipae wakati alipozindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)  kwenye ukumbi wa hoteli ya Midland Inn View jijini Dodoma, Januari 21, 2025.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Midland Inn View jijini Dodoma.


SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ikiwemo upande wa miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na kujenga uwezo wa wafanyakazi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo (Jumanne, Januari 21, 2025) alipozindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani wa “Systematic Observation Financing Facility (SOFF) - Project” katika Ukumbi wa Hotel ya Midland Inn View, Dodoma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la Serikali la kuendelea kufanya maboresho hayo ni kuwezesha utoaji wa utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.

Amesema miongoni mwa uwekezaji huo ni ununuzi wa rada saba za hali ya hewa, upanuzi wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na uboreshaji wa vifaa vya hali ya hewa kwa kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki kwa mujibu wa matakwa ya Mkataba wa Minamata.

Waziri Mkuu amesema, Serikali ya Tanzania katika kuunga mkono utekelezaji wa mradi wa SOFF imetenga fedha za kununua Vituo 11 vya Hali ya Hewa. Vituo hivyo vinavyojiendesha vyenyewe vitachangia data katika Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inaunga mkono kwa kutoa mchango wa zaidi ya dola za Marekani milioni nne ambazo ni thamani ya mchango kwa njia ya huduma zisizo za kifedha (In-Kind contribution). “Jitihada zote hizo, zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa.”

Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa mradi wa SOFF “SOFF - Investment Phase Project”, Mheshimiwa Majaliwa amesema mradi huo una umuhimu mkubwa siyo tu kwa kukidhi mahitaji ya data za hali ya hewa na tabianchi kwa ajili ya utabiri wa hali ya hewa duniani, bali pia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu ya Tanzania.

Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji na ubadilishanaji data za hali ya hewa kimataifa, hivyo kuimarisha huduma za hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa. “Mafanikio katika utekelezaji wa SOFF yatachangia sana kuimarisha ustahimilivu wa matukio ya hali mbaya ya hewa kwa maendeleo endelevu nchini”.

Amesema kuwa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea unategemea sana sekta zinazohusiana moja kwa moja na hali ya hewa, ambazo ni kilimo, lakini pia, ufugaji, nishati, maji, afya, madini na usafirishaji.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa iweke kipumbele cha kuboresha mtandao wa uangazi wa taarifa za hali ya hewa katika maeneo maeneo madogo madogo ambayo bado hayajafikiwa.

Agizo lingine alilolitoa kwa mamlaka hiyo ni pamoja na kuendelea kuimarisha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa zitakazosaidia kutoa huduma na kuboresha zaidi shughuli za kijamii na kiuchumi zinazofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

“Watumishi watakaopata  fursa ya kufanya kazi katika mradi wahakikishe wanafanya kazi kwa uadilifu na weledi ili utekelezaji wa mradi huo uwe na tija inayokusudia kwa Taifa letu. Waratibu wa mradi wahakikishe wanazingatia mpango mkakati wa utekelezaji wa mradi ili ukamilike kwa wakati na kwa ufanisi uanotarajiwa.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile amesema kwa sasa imani ya wananchi kuhusu masuala ya utabiri wa hali ya hewa imeongezeka na wanafuatilia taarifa za utabiri hali ambayo imesaidia kupunguza  majanga kwa kiasi kikubwa.

Amesema mradi wa SOFF utasaidia kuboresha miundombinu ya uangavu wa hali ya hewa, hivyo kuiwezesha nchi kufikia viwango vinavyohitajika katika utoa wa taarifa za hali ya hewa, ambapo utarahisisha uoakoaji wa watu na mali zao. Wizara itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha shughuli za TMA ili kufikia leo lililokusudiwa.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a ametaja faida za mradi huo unaogharimu Dola za Marekani zaidi milioni 13 kuwa ni pamoja na kuchangia kuongeza uwezo wa TMA katika utoaji wa huduma za hali ya hewa ikiwemo tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini na duniani kwa ujumla.

“Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuleta manufaa mbalimbali, ambayo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa nchini kupitia ununuzi wa vituo vipya tisa vya kisasa vya uangazi wa Hali ya Hewa vinavyojiendesha vyenyewe, vituo vitatu vya uangazi wa anga za juu na maboresho ya vituo saba vya uangazi vinavyojiendesha vyenyewe na kituo kimoja cha uangazi wa anga za juu.”

Pia, Dkt. Chang’a amesema manufaa mengine uboreshaji wa huduma za tahadhari zitakazosaidia shughuli za kiuchumi na kupunguza hatari za majanga pamoja na kukidhi matakwa na mahitaji ya kimataifa kama Mtandao wa Uangazi wa Msingi wa Kimataifa.

Amesema TMA ni miongoni mwa Taasisi bora za Hali ya Hewa barani Afrika zinazoaminika na kutumiwa na WMO kutoa msaada wa kiufundi kwa nchi nyingine barani Afrika ikiwa ni pamoja na katika Mfumo wa Kusimamia Ubora (QMS), Mpango wa Pamoja wa Kutoa Tahadhari (CAP) na Utabiri wa Hali ya Hewa kwa njia ya Modeli za Kompyuta (NWP).

Awali, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya SOFF, Markus Repnik aliipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa iliyoufanya kwa TMA na kwamba wataendelea kushirikiana nayo katika kuhakikisha harakati za kuimarisha uangazi wa hali ya hewa zinafikiwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi alipowasili kwenye  hoteli ya Midland  Inn View jijini Dodoma kuzindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Januari 21, 2025. Wa pili kuila ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule,  wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa  Uchukuzi, David Kihenzile na wa  nne  kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ngoma  alipowasili hoteli ya Midland  Inn View jijini Dodoma kuzindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Januari 21, 2025.  Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi , David Kihenzile.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na viongizi wengine wakiwa wamesimama wakati Wimbo wa Taifa ulipoimbwa katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)  kwenye ukumbi wa hoteli ya Midland Inn View jijini Dodoma, Januari 21, 2025.  Kulia kwake  ni Naibu Waziri wa Uchukuzi , David Kihenzile,   kushoto kwake ni Kaimu   Mkurugenzi wa  Mamlaka ya Hali ya Hera Tanzania, Dkt. Ladislaus Chang’a na kushoto ni Mkuu wa Moa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Midland Inn View jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza nao kwenye ukumbi wa hoteli ya Midland Inn View jijini Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark, Bi Marriane Thrilling baada ya kuzindua  Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)  kwenye ukumbi wa hoteli ya Midland Inn View jijini Dodoma, Januari 21, 2025.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

















 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMANNE, JANUARI 21, 2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.