Menu

Friday, June 6, 2025

WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TUME YA UTUMISHI WA WALIMU KUTENDA HAKI ILI IWE KIMBILIO LA WALIMU.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Ummana Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akizungumza  wakati akifunga mafunzo ya  Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu yaliyofanyika kwa muda wa  siku tatu  katika Chuo Cha Utumishi wa Umma, Tanzania, Kampasi ya Tabora yaliyoendeshwa na TSC.

Baadhi ya Maafisa Elimu walioteuliwa kuwa Wajumbe wa Kamati za Ajira, Upandishaji Vyeo na Nidhamu wa Tume ya Utumishi wa Walimu ngazi ya Wilaya wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Ummana Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene wakati akifunga mafunzo ya  Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu yaliyofanyika kwa muda wa  siku tatu  katika Chuo Cha Utumishi wa Umma, Tanzania, Kampasi ya Tabora yaliyoendeshwa na TSC.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Walimu (TSC) Prof. Masoudi  Muruke akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene kwa ajili ya  mafunzo ya  Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu yaliyofanyika kwa muda wa  siku tatu  katika Chuo Cha Utumishi wa Umma, Tanzania, Kampasi ya Tabora yaliyoendeshwa na TSC.
Na Lusungu Helela - TABORA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema anatamani  kuona Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) inakuwa kimbilio la Walimu ambao ni kundi kubwa katika Utumishi wa Umma kwa kutenda haki pindi inaposhughulikia  mashauri ya nidhamu na rufaa za Walimu

 

Amesema haifurahishi kuona Walimu wanapoteza ajira kwa ukiukaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma ilhali TSC ipo.

 

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo  wakati akifunga mafunzo ya  Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu yaliyofanyika kwa muda wa  siku tatu  katika Chuo Cha Utumishi wa Umma, Tanzania, Kampasi ya Tabora yaliyoendeshwa na TSC.

 

Amesema TSC ndiyo mlezi wa Walimu, hivyo Wajumbe na watumishi wa Tume hiyo watoe elimu kwa Walimu katika masuala muhimu yanayohusu utumishi wao kwa kuzingatia jukumu lake la ulezi, adhabu ya kufukuzwa  kazi iwe ni hatua ya mwisho pale inapotokea Mwalimu kutotii yale anayoelekezwa.

 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amewataka Maafisa  Elimu walioteuliwa kuwa Wajumbe wa Kamati za Ajira, Upandishaji Vyeo na Nidhamu wa Tume ya Utumishi wa Walimu ngazi ya Wilaya wakatumie mafunzo hayo waliyoyapata  kama nyenzo ya kuboresha utendaji kazi kwa kutoa haki kwa Walimu wenye mashauri ya nidhamu na rufaa.

 

" Ni matumaini  yangu kuwa baada ya mafunzo haya hatutasikia au kuona uamuzi wa shauri unakatiwa  rufaa Tume ya Utumishi wa Walimu Makao Makuu kwa kuamuriwa bila kuzingatia matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu  zinazowaongoza katika kufikia uamuzi kwa haki na usawa" amesema Mhe.Simbachawene.

 

 

Vile vile Mhe. Simbachawene ametoa rai kwa Wajumbe hao kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia uendeshaji wa mashauri ya nidhamu pindi wamaposhughulikia mashauri ya nidhamu na rufaa.

 

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu Prof. Masoudi  Muruke amesema lengo la mafunzo hayo ni  kuhakikisha kunakuwa  na Walimu ambao wanajituma na wanaozingatia maadili ya kazi yao kwa ajili ya kuwalea watoto kwa usahihi na hivyo kuboresha elimu nchini kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

 

Mwisho

No comments:

Post a Comment