Na.Mwandishi OMKR Zanzibar
Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman amesema licha ya juhudi zinazochukuliwa na
serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuimarisha haki za jamii ya watu wenye ulemavu,
bado yapo mahitaji mengi na kupitia maradi CADiR nchi itaongeza uwezo wa kulifikia vyema kundi
hilo ili kuimarisha upatikanaji huduma, haki na fursa za kimaendeleo kwa watu
hao.
Hayo ameyasema huko hoteli ya Madinat Al Bahar Mbweni Mjini
Zanzibar alipozungunza katika ufunguzi rasmi wa mradi wa miaka mitano wa kukuza
na kuimarisha utoaji wa haki za watu wenye Ulemavu (CADiR), unaozishirikisha
taasisi za serikali, asasi za kiraia na Binafasi nchini.
Hvyo, mhe. Othman ametoa wito kwa jamii nchini kwamba ni vyema kila mmoja kulichukulia suala la haki
na fursa za watu wenye ulemavu ni
jambo la wajibu, sio tu kwa serikali, lakini kwa watu wote na linakuwa sehemu ya utamaduni wa wananchi na
linalohitaji mashirikiano kutoka kila mtu
na kujenga jamii bora yenye ustawi.
Mhe. Othman amefahamisha kwamba kwa kutambua umuhimu wa mradi
huo ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar itaendelea kutoa mashirikiano
ya kutosha katika kuhakikisha unafanikiwa
kama ilivyopangwa na kufikia leo
la jamii jumuishi.
Kuhusu suala la watu wenye ulemavu kutumika kuwa omba omba
Mhe. Othman amesema kwamba sharia kuhusu suala hilo inasema wazi kwamba ni kosa
la jinai kuwatumia watu wa aina hiyo na kwamba kwa kuwa suala hilo lipo sana
Mkoa wa mjini Magharib serikali za wilaya na mkoa wanayo mamlaka ndani ya wiki
moja kuliondosha jambo hilo.
Amesema kwamba ni muhimu kwa viongozi katika jambo hilo
ambalo linawadhalilisha watu wenye ulemavu kutolitia siasa na badala yake
sharia ichukue nafasi yake katika kuikabili na kulimaliza ndani ya kipindi
kifupi bila kuangaliwa watu machoni.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Mhe. Harous Said Suleimani akimkaribisha Mhe. Makamu amemshukuru
kwa jitihada zake za kufanya kazi kwa kuwashirikisha jambo0 ambalo limesaidia
kupatikana ufanisi kwenye masuala mbali mbali kiutendaj.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Zanzibar
(SHIJUWAZA) Mwandawa Khamis Mohammed, amesema kwamba jumuiya hiyo itajitahidi katika
kuhakikisha kwamba inatoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo wa
kuimarisha haki kwa watu wa jamii hiyo na malengo yaweze kufikiwa.
Ametoa wito kwa Watu wenye ulemavu
kuwa tayari katika kuzichangamkia fursa mbali mbali zinazotolewa kupitia mradi
huo na kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyote katika jumuiya hiyo anayeachwa
nyuma kwenye manufaa ya mradi huo.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la
watu wenye ulemavu kutoka Tanzania Bara Tungi Mwanjala, amesema kwamba uzinduzi wa mradi huo ni tukio walilolisubiri
kwa muda mrefu na kwamba mjumuiko huo unatoa matumaini katika kuhakikisha
kwamba mradi huo unatekelezwa katika kufikia maisha mazuri kwa watu wenye
ulemavu.
Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Mradi huo
hapa Zanzibar ndugu Abdalla Omar, amesema kwamba Progaram hiyo imefadhiliwa na
serikali ya Norway kupitia shirika lao la Maendeleo la NORAD na kuzishirikisha Taasisi
tano kutoka nchini humo zinazoshughulikia maendeleo ya watu wenye ulemavu.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Watu wenye Ulemavu Zanzibar Mhandisi Ussi Khamis Debe akiwatambulisha wageni kwenye uzinduzi huo, amesema kwamba mradi huo utasaidia kujenga misingi imara zaidi ili kuondosha vikwazo kwa jamii hiyo na kuweza kufikia dira ya kujenga jamii jumuishi katika shughuli zote za maendeleo nchini.
Mradi huo muhimu kwa Maendeleo ya Watu wenye Ulimavu unalenga katika utoaji wa elimu mjumuisho , uwezeshaji kiuchumi, afya na marekebisho,na pia uhamasishaji na utetezi wa haki za watu wenye ulemavu ambao unatekelezwa kwa Tanzania Bara na Zanzibar unathamani ya zaidi ya shilingi 20 bilioni za Tanzania.
Mwisho
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
kupitia Kitengo chake cha habari leo Jumatano tarehe 20 Agosti 2025.
No comments:
Post a Comment