Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali imeweka kipaombele cha kuwapitia huduma bora za afya wananchi wote wa Zanzibar.
Ameyasema hayo katika uzinduzi wa kambi ya tano ya matibabu ya ‘Afya bora maisha bora’ uliyofanyika katika viwanja vya hospitali ya Wilaya Vitongoji, Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), imejikita kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta mbali mbali zikiwemo afya na uwekezaji.
Mhe. Hemed amesema utoaji wa huduma bure za matibabu kwa jamii kupitia kambi hiyo sio tu sehemu ya kufikisha huduma za afya kwa lengo la kujenga jamii yenye afya bali pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025.
Aidha, amesema kambi hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma za tiba za dharura na maabara ya kisasa na kuendeleza mageuzi makubwa katika sekta ya afya, akisema kambi nne zilizopita, zaidi ya watu 21,000 walifikiwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amempongeza Mwenyekiti na Msarifu wa ZMBF, mama Mariam Mwinyi, kwa namna alivyobaini changamoto zilizopo katika jamii na kuamua kujitolea kuwafikishia huduma za matibabu bure wananchi.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa watendaji wa taasisi za serikali, binafsi na wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kambi hizo zinafanikiwa na kutekelezwa kwa ubora, umahiri na viwango.
Amewataka wanachi kuendelea kutumia huduma za afya zinazotolewa na serikali na wadau kwa kuwa ni haki yao na fursa ya kila mtu na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika kuimarisha huduma muhimu kwa jamii.
Mhe. Hemed amewakumbusha wanchi umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano na kushiriki uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba 2025 na kuwasihi kutokubali kutumika kuvuruga amani kwa maslahi ya watu wachache wasioipendelea mema Zanzibar na Tanzania.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Mngereza Mzee Miraji, amesema kambi hiyo imeandaliwa kwa pamoja kati ya serikali na ZMBF kwa lengo la kukuza huduma za afya za msingi kwa wananchi.
Amefahamisha kuwa kampeni hiyo imelenga kupambana na changamoto za maradhi yakiwemo ya kuambukiza, huduma za kibingwa za macho, meno, watoto na wanawake na upasuaji.
Amesema kambi hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa zaidi ya wananchi 5,000, kupunguza utapia mlo na kuimarika kwa viashiria vya afya.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZMBF, Fatma Fungo, amesema lengo la kambi hiyo ni kuimarisha huduma za afya za msingi katika ngazi ya jamii na kuhakikisha maisha yenye afya na ustawi kwa wote.
Fungo amesema kambi kama hiyo zimeshafanyika kwa mikoa minne ya Zanzibar na kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 21,000 na kwa sasa wapo tayari kuwahudunia wananchi wa mkoa wa Kusini Pemba kwa kuwapatia huduma za afya zitakazotolewa bila ya malipo kuanzia Agosti 11 hadi Agosti 15.
Amesema matarajio ya kambi hiyo ni kuwahudumia wananchi wengi wa mkoa huo na kuhakikisha lengo la kuwahudumia wannachi zaidi ya 25,000 linafikiwa.
Nao wananchi waliofika kupatiwa matibu, wakiwemo Asha Wahid Juma na Ali Kombo Ali, wameeleza kufarajika na kunufaika na kambi hiyo ambao wamepata fursa ya kuchunguza na kupima afya zao na kupatiwa matibabu bila ya malipo.
Wameiomba Wizara ya Afya Afya na ZMBF, kuziendeleza kambi hizo kwani ni mkombozi mkubwa kwa wananchi hasa wa vijijini na wazee.
Kambi hiyo inatarajiwa kufungwa kwa kuhusisha matembezi ya Mariam Mwinyi Walkathon, yatakayoongozwa na mama Mariam Mwinyi.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR)
Tarehe 12.08.2025
No comments:
Post a Comment