MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akimuombea kura Mgombea wa Ubunge jimbo la Musoma Mjini Ndg. Mgore Miraji Kigera katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mkendo Musoma.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira Amezindua kampeni za CCM katika jimbo la Musoma mjini lenye kata 16 ambapo kata mbili kati ya hizo wagombea udiwani wa chama hicho wamekosa wapinzani.
Ndg. Wasira amewataka watu wanaohoji kwanini wanamsifia Mwenyekiti wa chama hicho Samia Suluhu Hassan kuacha kulalamika badala yake nao wafanye mambo mazuri ya maendeleo ili wasifiwe.
Amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake Rais Samia amefanya mambo makusuala.labwa ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii ikiwemo katika sekta za afya,maji, elimu na sekta zingine na kwamba chama chake bado kinalenga kufanya mambo mengine makubwa kwa wananchi.
Akizungumza mjini Musoma leo Septemba 6,2025 kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika jimbo la Musoma Mjini, Wasira amesema lengo la chama hicho ni kuendelea kushika dola ili kuwatumikia wananchi na ndio maana wameandaa ilani bora yenye kujibu mahitaji na changamoto zete za wananchi.
"Sasa wanalalmika nini wakati hawana chochote walichokifanya,sisi lazima tumasifie wa kwetu kwasababu amefanya mengi sana na tunayaona,sasa wewe unalalamika wakati hata zahanati haujajenga,fanya maendeleo na wewe usifiwe kwasasa tuko na mama Samia," amesema.
Wasira amesema chama hicho kina malengo mazuri na wananchi na ndio maana kimerudi tena kuomba ridhaa ya kushika dola huku akisema katika jimbo la Musoma mjini na mkoa mzima wa Mara yapo mengi mazuri yaliyopangwa kufanyika kwa maslahi ya wakazi wa jimbo hilo.
Amesema miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kufanywa na chama hicho katika Mkoa wa Mara kwa ujumla ni pamoja ujenzi wa vituo vya afya vipya 18, zahanati mpya 37 pamoja na huku sekta ya elimu na zingine zikitarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa.
Kuhusu uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa mkoa kwa ujumla ,Wasira amesema yapo mengi yanayotarajiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari ya Musoma sambamba na kuimarishwa kwa sekta ya kilimo kwa kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji ili wananchi waachane na kilimo cha kutegemea mvua.
"Kwakweli mambo ni mengi nikianza kutaja kila kitu hapa basi tutalala Mukendo itoshe kusema tuna mipango mizuri sana na nyie, tutakwenda kufufua viwanda na kila kitu ili mradi uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa mkoa uimarike," amesema
Wasira amesema licha ya uwepo wa watu wanaodai kuwa chama hicho hakijafanya chochote katika maisha ya watanzania lakini ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo mengi yamefanyika na ndio maana chama hicho kinaendelea kupata ujasiri wa kuomba ridhaa kwa wananchi.
"Tukisema tuwafufue wale waliokuwepo hapa miaka ya 61 hakika wakija watasema hii sio Musoma kwani maendeleo ni mengi sana mfano miaka minne ya Samia amejenga shule mpya za Sekondari tatu, madarasa 98 ya shule za Sekondari na madarasa 68 katika shule za Msingi, kituo kimoja cha afya na zahanati tatu," amesema
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Benedict Magiri amesema wana CCM ndani ya wilaya hiyo wana mshikamno kwa asilimia 89 baada ya kuvunjwa kwa makundi yaliyotokana na mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
"Tumepita kwenye kata zote 16 za Manispaa ili tusemane,tuzungumze na tuwekane sawa lengo kuu likiwa ni kuvunja makundi ili wana CCM tuimbe wimbo mmoja wa Chama cha Mapinduzi,' amesema
Amesema anaamini kwa vikao hivyo walivyofanya wanachama wa chama hicho sasa hivi wameshikamana na kwa pamoja wanatafuta kura za chama kuanzia urais hadi udiwani.
Mgombea ubunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji amewaomba wakazi wa jimbo hilo kukipigia kura chama cha Mapinduzi huku akisema changamoto zote za wakazi wa jimbo hilo zinakwenda kupatiwa ufumbuzi.
"Changamoto kubwa ya Musoma ni ajira na uchumi niwaombe nyie mniachie hilo jukumu nyie kazi yenu ni kumchagua Mgore, mama Samia na madiwani wote wa CCM halafu muone tutakayofanya," amesema
Mgore amesema ili kupata suluhisho la kudumu katika changamoto hizo suala la uwekezaji na ufufuaji wa viwanda litapewa kipaumbele huku akisema kazi ya kuwatafuta wawekezaji ataifanya yeye mwenyewe na kuiomba serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Iddi Mkowa amesema chama hicho kinaamini katika utawala wenye kuzingatia usawa wa wa kijinsia kwa vitendo na kwamba katika kuhakikisha hilo linafanikwa wagombea ubunge katika majimbo manne kati ya kumi yaliyopo mkoani humo ni wanawake.
Ameyataja majimbo hayo na wagombea wake kuwa ni pamoja na Mgore Miraji(Musoma Mjini), Mary Daniel (Serengeti), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Esther Bulaya (Bunda Mjini).
Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), Gaudensia Kabaka amesema hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho kusimamisha wagombea wengi wanawake kwa nafasi ya jimbo mkoani Mara.
"Hii haikuja kwa bahati mbaya wote tunajua Mkoa wa Mara ulikuwa na sifa gani kuhusu wanawake lakini kazi imefanyika na kwasasa tunaona matunda, niipongeze kamati kuu kwa kazi nzuri haikuwa rahisi lakini hakika wameweza," amesema
Amesema wagombea wote walioteuliwa na chama hicho wana sifa na wanafaa kuwa wawakilishi wa wananchi huku akiwataka wakazi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kukichagua Chama cha Mapinduzi Oktoba 29,2025.
Mgombea ubunge Tarime Mjini, Esther Matiko amesema Mkoa wa Mara umeongoza nchini kwa kuteuwa idadi kubwa ya wagombea wanawake kwenye majimbo jambo ambalo halikuwahi kutokea huko nyuma.
Amesema uteuzi wa wagombea wanne wa nafasi hiyo katika majimbo hayo ni sawa na asilimia 40 na kwamba katika historia ya mkoa huo haijawahi kutokea kuwepo kwa wagombea wengi wanawake na kuahidi kuwa endapo watachaguliwa watashirikiana na wabunge wengine pamoja na madiwani wote kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa kwa asilimia 100.
"Mara huko nyuma tulikuwa tukitambulika kama mkoa ambao hauthamini wanawake hasa kwenye masuala ya uongozi lakini CCM chini ya Rais Samia imeidhihirishia dunia kuwa Mara tunaweza kilichobaki ni kupiga kura ili tufanye kwa vitendo," amesema Matiko
Aliyekuwa Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo amesema hana shida na maamuzi yaliyofanywa na chama chake kwa maelezo kuwa chama hicho ni kikubwa zaidi ya mtu binafsi.
Jina la Mathayo lilikatwa katika hatua za awali kabla ya mchakato wa kura za maoni jambo ambalo kwa namma moja ama nyingine lilisababisha makundi ndani ya chama hicho katika jimbo la Musoma mjini.
"Wanaosema nina kundi sio kweli kwanza mimi sikuwa mgombea lakini pia najivunia kufanya kazi na marais wanne na muda wote tumeleta maendeleo yanayoonekana kwa macho na ni kwa faida ya jimbo letu hivyo sina kinyongo na maamuzi ya chama changu zaidi najivunua maendeleo yaliyopatikana wakati wa uongozi wangu," amesema
Mathayo amesema chama chao ni kama kocha wa mpira wa miguu ambaye anaamua ampange mchezaji gani kwa wakati gani hivyo mchezaji hawezi kuhoji kwanini hajapangwa kucheza.
"Mchezaji usipopangwa kuna mawili aidha kiwango chako kimeshuka au umewekwa akiba ila mimi naamini nimewekwa akiba kwahiyo sina wasiwasi wala kinyongo," amesema
No comments:
Post a Comment