6/recent/ticker-posts

SALAMU ZA PONGEZI ZAANZA KUMIMINIKA KUMPONGEZA DK SHEIN - RAIS WA ZANZIBAR

Na Rajab Mkasaba

SALAMU za pongezi kutoka ndani na nje ya Tanzania zinaendelea kutolewa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar wa awamu ya saba.



Salamu hizo za pongezi zinatoka kwa Jumuiya, Vyama vya Siasa, Mashirika, Wizara, Taasisi za serikali na zisizo za serikali, afisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo nchi za nje, watu binafsi na wananchi mbali mbali.



Miongoni mwa salamu hizo ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambazo zilieleza kuwa nafasi ya Urais aliyoipata Dk. Shein inastahiki na uongozi na wanachama wa CCM wamefurahishwa na matokeo ya uchaguzi huo na Chama kinaamini kuwa chini ya uongozi wake Zanzibar itapiga hatua kubwa katika maendeleo.



Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo ilimtakia kika la heri na mafanikio Dk. Shein katika kazi yake mpya ya Urais wa Zanzibar na kumpongeza kwa ushindi alioupata.



Nao Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman ulieleza kupokea kwa furaha kubwa kwa kuchaguliwa Dk. Shein kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 31,2010.



Ubalozi huo ulieleza kuwa kuchaguliwa huko kwa Dk. Shein ni dhahiri kunatokana na imani waliyonayo Wazanzibari juu ya uongozi wake na uwezo wa Chama Cha Mapinduzi katika kuwaletea maendeleo na maisha bora kwa Ari zaidi, Nguvu zaidi na Kasi zaidi wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.



Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden nao umetoa salamu za pongezi kwa niaba ya Watanzania wote walioko Sweden, Denmark, Norway, Finland, Latvia, Estonia, Lithuania na Iceland na kueleza pongezi zao za dhati kwa Dk. Shein kwa kufanikiwa kupata ridhaa za Wazanzibari kuweza kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.



Aidha, kwa niaba ya wafanyakazi wote wa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dubai na Emarat za Kaskazini za UAE wametoa salamu za pongezi kwa Dk. Shein kwa ushindi mkubwa alioupata na kumuombea kila la kheri na mafanikio mema katika majukumu yake mapya.



Ubalozi wa Tanzania nchini China nao umeleta salamu za pongezi kwa Dk. Shein na kumtakia kila na heri katika kazi yake mpya ya Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.



Nao Mfuko wa Mwalimu Nyerere umetoa salamu za pongezi kwa Dk. Shein kwa kuwa Rais wa Zanzibar mpya itakayokuwa na sura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo inawakilisha wananchi wote wa Zanzibar.



Nayo Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar (JUWAZA), imetoa salamu za pongezi kwa Dk. Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais Muanzilishi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.



Salamu za Pongezi kutoka kwa jumuiya hiyo zilimtakia kila la heri Dk. Shein na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe uwezo, maarifa na hekima katika uongozi wake na kuipeleka Zanzibar katika pahala inapostahili na kudumisha amani, utulivu na maendeleo zaidi.



Dk. Ali Mohammed Shein ameshinda nafasi ya Urais baada ya kujipatia ushindi wa jumla ya kura 179,809 sawa na asilimia 50.1, katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu.



Katika kinyang’anyiro hicho cha kugombea wa Urais Zanzibar, Dk. Shein alimshinda mgombea wake wa karibu kutoka chama cha CUF, Seif Sharif Hamad aliyepata kura 176,338 ambazo ni sawa na asilimia 49.1.

Post a Comment

0 Comments