Na Khamis Amani
MTUHUMIWA wa kesi ya kuchoma moto msahafu pamoja na juzuu za dini ya Kiisilamu katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, ametakiwa kujibu shitaka hilo.
Hatua hiyo ni baada ya mahakama inayosikiliza kesi hiyo kumuona kuwa analo shitaka la kujibu kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashitaka uliowasilishwa mahakamani hapo.
Akitoa uwamuzi mdogo wa kesi hiyo (ruling), hakimu wa mahakama hiyo Khamis Ali Simai alisema kuwa, baada ya kupitia kwa kina ushahidi huo, mahakama imemuona kuwa ana shitaka la kujibu.
"Mahakama baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashitaka imeweza kuridhishwa na kujenga kesi hii, hivyo mtuhumiwa utatakiwa kujibu shitaka linalokukabili", alisema hakimu Khamis Ali Simai.
"Hivyo chini ya kifungu cha 215 (1) cha sheria, sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar, utatakiwa kujibu shitaka hilo", aliongeza.
Baada ya mahakama hiyo kumuelewesha haki zake za utetezi ikiwemo cha kiapo na bila ya kiapo, mtuhumiwa huyo alisema atajitetea kwa kiapo pamoja na kumuwasilisha shahidi mmoja mahakamani hapo.
Hivyo, baada ya hatua hiyo, hakimu Khamis Ali Simai alilazimika kuiahirisha kesi hiyo hadi Febuari 7 mwaka huu, na mtuhumiwa amerejeshwa tena rumande kwa kile kilichoelezwa ni usalama wa maisha yake.
Jumla ya mashahidi sita wa upande wa mashitaka akiwemo mpelelezi wa kesi hiyo ya jinai namba 432/2010 Z 2189 Sajenti wa Polisi Suleiman wa Kituo cha Polisi Mazizini wamesikilizwa na mahakama hiyo ya wilaya.
Mtuhumiwa wa kesi hiyo ni Ramadhani Handa Tuma (28) mkaazi wa Mombasa wilaya ya Magharibi Unguja, ambaye anakabiliwa na mashitaka ya kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani pamoja na kukashifu dini.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Novemba 18 mwaka jana na kusomewa mashitaka hayo na Mwanasheria wa serikali kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Khamis Jaffar Mfaume, ambayo aliyakanusha.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, kinyume na kifungu cha 74 (1) (b) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, Novemba 16 mwaka jana alifanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.
Mahakama ilifahamishwa kuwa siku hiyo, mahala hadharani kwa makusudi na bila ya halali alichoma moto msahafu pamoja na juzuu za dini ya Kiisilam, kitendo ambacho kilidaiwa kuwa kingeweza kuleta uvunjifu wa amani kwa jamii ya dini ya Kiislamu.
Tukio hilo lilidaiwa kutokea huko Mombasa wilaya ya Magharibi Unguja, majira ya saa 2:30 za usiku.
Sambamba na shitaka hilo, pia alidaiwa kuikashifu dini hiyo ya Kiisilamu kwa kuchoma moto vitabu hivyo, kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 117 na 27 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
2 Comments
kwa usa;lama wake huyo mfungeni laa si hivyo atajuta kuw ahuru. na pia tusimuone katika kisiwa cha zanzibar yaani unguj ana pemba na haishii hapo na ukanda wa pwani yote ya africa mashariki na kati. mwacheni aende huko huko kwa dr slaa. mshenzi mmoja
ReplyDeletechonde chonde tuiachie sheria ichukue mkondo wake
ReplyDelete