6/recent/ticker-posts

ZSSF YAWASEMEA WAFANYAKAZI SEKTA YA ULINZI

Na Haji Mtumwa

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) umewashauri wakuu wa kampuni za Ulinzi kuwahamasisha wafanyakazi wao ili kujiunga na mfuko huo.

Ofisa Uhusiano wa Mfuko huo Raya Hamdan Khamis, alieleza hayo alipozungumza na Mwandishi wa habari hii ofisini kwake Kilimani Mjini Zanzibar.

Alisema kuwa ni vyema kwa waajiri wa kampuni hizo wakawahimiza wafanyakazi wao kufika ofisini hapo kwa lengo la kujiunga na Mfuko huo ili kuwawezesha kutambua vyema haki zao zilizopo katika Mfuko huo.

Alifahamisha kuwa wafanyakazi wengi wa kampuni hizo wamekuwa wakifika ofisini hapo kwa lengo la kuangalia akiba zao na kutozikuta kutokana na kukosa kujiunga na Mfuko huo.

Alisema inawezekana wafanyakazi wengi hawazifahamu taratibu za Mfuko huo kabla ya kuangalia akiba zao au kuuliza kwa waajiri wao kanuni za Mfuko wa Hifadhi ya jamii Zanzibar (ZSSF).

Kauli ya ofisa huyo imekuja kufuatia kuwepo kwa malalamiko kwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za Ulinzi wakidai kunyimwa haki zao, zikiwemo za kutofikishiwa fedha zao Mfuko wa Hifadhi ya jamii.

Wafanyakazi hao walisema waajiri wao wamekuwa wakiwakata asilimia 5, ya mishahara yao kila mwisho wa mwezi kwa lengo la kuwafikishia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), lakini fedha hizo hawazioni wakifika katika Mfuko huo.

Pamoja na kauli za wafanyakazi hao lakini kwa upande wa kiongozi mmoja wa kampuni za Ulinzi Ashraf James, alisema kauli za wafanyakazi hao si za ukweli hata kidogo.

Kiongozi huyo alifahamisha kuwa wengi wa wafanyakazi ambao wenye madai hayo ni wale ambao hawajatekeleza masharti ya kujiunga Mfuko huo, hivyo upande wao hawawezi kuwekekwa akiba hadi pale watakapokamilisha taratibu za kujiunga.

Mkurugenzi Idara ya Kazi, Iddi Ramadhan Mapuri pamoja na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Majumbani, Mahotelini na sehemu nyengine Makame Launi Makame, kwa nyakati tofauti walisema kuwa hali hiyo wanaifahamu na tayari wameshachukua hatua.

Walisema kuwa miongoni mwa hatua hizo ni kuandaa mikakati madhubuti ya upatikanaji wa haki za wafanyakazi na kukomesha vitendo viovu juu yao na kuwafanya kuwa katika hali ya usalama na utulivu katika sehemu zao za kazi.

Post a Comment

0 Comments