Na Haji Nassor, Pemba
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa amewakaribisha wafanyabiashara kuwekeza vitega uchumi kisiwani humo kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika na miundombinu ya kuaminika ikiwa ni pamoja na barabara.
Alisema kwa sasa kisiwa cha Pemba kimeshapiga hatua kubwa ambayo inatoa taswira bora kwa mazingira ya wawekezaji ambayo hapo kabla hayakua rafiki kwa wawekezaji hasa kutokana na kutoa kua na umeme wa
uhakika.
Tindwa alitoa tamko hilo jana kwenye hafla ya ufunguzi wa mkahawa Samail hapo mjini Chake Chake, ambapo alieleza kwa sasa Pemba ina mazingira bora ya uwekezaji.
Alieleza kwa muda mrefu baadhi ya wawekezaji walikuwa na hamu ya kuekeza Pemba na kushindwa kutokana kutokuwepo kwa miundombinu rafiki, lakini kwa sasa hali hiyo imebadilika na ina tia moyo.
“Kwa sasa hali ya uwekezaji kisiwani Pemba inatia moyo na inakubalika hasa tokea serikali ituwekea umeme wa uhakika na kuwepo kwa miundombinu ya kisasa ikiwani pamoja na barabara, mawasiliano na huduma ya maji safi na salama’’,alieleza Tindwa.
Akizungumzia kuhusu mkahawa huo alisema amefarajika sana kuona umejengwa ndani ya Mkoa wake ambapo utasaidia kuondoa usumbufu uliopo wa kutokuwepo kwa maeneo ya kisasa ya kula chakula kwa wageni wanaofika kisiwani Pemba.
Aliongeza kuwa pia mkahawa huo utasaidia kunawirisha mji wa Chake Chake na Mkoa wa Kusini Pemba kwa ujumla kwa kuwepo kwa eneo hilo ambalo limekua la kisasa kwa kutoa huduma za chakula.
Mapema Mkuu wa wilaya ya Chake chake Mwanajuma Majid Abdallah alisema wilaya imefarajika sana kuona muekekezaji huyo ameamua kufungua mkahawa huo ambao pia utatoa huduma ya chakula na kuongeza pato la serikali.
Mwanajuma alieleza kua wakati umefika kwa wawekezaji kutuimia fursa ya kuimarika kwa miundombinu mbali mbali kisiwa Pemba kuekeza kwani bado wananchi na wageni wanaotembelea kisiwani humo wanahitaji huduma za aina mbali mbali.
Akisoma risala kwenye hafla hiyo mmoja kati ya uongozi wa mkahawa huo Nassor Humud alisema wameamua kuekezea kisiwani Pemba pamoja na biashara pia kuwapatia huduma wenyeji na wageni wanaotembekea Kisiwani humo.
Alifafanua kuwa kwa sasa kisiwa cha Pemba kimeimarika kwa kuwepo kwa huduma ya umeme wa uhakika na mindombinu ya barabara ambayo haina usumbufu kama ilivyokua hapo awali.
0 Comments