ILI kuweka mazingira mazuri ya umiliki na matumizi ya ardhi, serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara ya Ardhi, Makaazi, Ujenzi na Nishati, inajiandaa kuandika upya sera ya ardhi baada ya iliyopo kupitwa na wakati.
Hata hivyo, kabla kuandika sera hiyo, kumeundwa kamati ya watu 14 kufanya utafiti na mashauriano na sekta mbalimbali ambazo utendaji wao kwa namna moja au nyengine unahusiana na masuala ya ardhi.
Aidha, wananchi wa maeneo mbalimbali watashirikishwa kutoa maoni kwa mikutano na njia tafauti za mawasiliano, ambapo shughuli hiyo inafadhiliwa na Serikali ya Finland kupitia mradi wa SMOLE.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo katika ukumbi wa wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Shangani mjini Zanzibar jana, Mshauri wa Uongozi na Usimamizi wa Ardhi katika mradi wa SMOLE, Pertti Onkalo, alisema kwa kuwa ardhi ni rasilimali muhimu, utafiti huo ufanywe kwa kuwahusisha wadau na wananchi kwa jumla.
Alisisitiza haja ya kuzingatia dira na malengo, pamoja na mahitaiji yote muhimu katika uendelezaji wa ardhi ili sera mpya itakayoandikwa iwe na manufaa kwa kila raia wa nchi pamoja na wawekezaji.
Aidha alisema, kupitiwa kwa sera hiyo na kuifanyia marekebisho, kutahakikisha ufanisi katika dira ya serikali kutokomeza umasikini ifikapo mwaka 2020.
Alieleza kuwa, ardhi ni mali yenye umuhimu mkubwa hasa kwa watu walio masikini, wanawake na makundi maalumu, hivyo ni vyema uandikaji wa sera mpya uzingatie mahitaji hayo.
“Kila raia wa nchi ana haki ya kupata sehemu ya ardhi, ili ajiletee maendeleo yatakayosaidia kuondokana na umasikini, hata wawekezaji nao watanufaika kama kutakuwa na sera inayotekelezeka, ni vyema tuifanye kazi hii kwa kutambua umuhimu huo”, alifafanua Onkalo.
Naye Mkurugenzi Utumishi katika wizara ya Ardhi, Makaazi, Ujenzi na Nishati Fatma Ali Suleiman, alisema kutokana na sera ya mwaka 1982 kupitwa na wakati, na kushindwa kufanya kazi ipasavyo, sera mpya italeta matumaini na utulivu kwa wamiliki wa ardhi na serikali kwa jumla.
Alisema katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, kumejitokeza matatizo mengi na migogoro ya ardhi ambayo kwa kiasi kikubwa imesababishwa na mapungufu yaliyomo ndani ya sera ya zamani.
“Tunatumai sera mpya ya ardhi itakuwa mkombozi pamoja na kuweka mazingira mazuri kati ya wananchi na wawekezaji ambapo mara kadhaa wamejikuta wakiingia katika mivutano isiyo ya lazima”, alieleza.
Kwa upande wake, ofisa kutoka Kamisheni ya Utalii, Said Abdulrahman, alisema tangu serikali ifungue milango kwa wawekezaji katika sekta ya utalii, pamoja na mafanikio, lakini kumekuwa na matatizo yanayosababisha migogoro na kuwakimbiza baadhi ya wawekezaji.
Hata hivyo, alisema kuundwa upya kwa sera ya ardhi, ni njia muafaka ya kumaliza hali hiyo na kuvutia wawekezaji zaidi pamoja na wananchi wanaomiliki ardhi kuzingatia sheria wakati wa kuitoa kwa ajili ya uwekezaji.
Jumla ya watu 14 kutoka taasisi mbalimbali za umma, wameteuliwa kuunda kamati hiyo, ambapo itakuwa ikifanya vikao na wadau wengine katika kuandaa sera hiyo.
1 Comments
Jambo la maana sana!..lkn. hatukutarajia kua kwa wasomi na wanasiasa hodari tulionao tutasubiri mpaka mzungu aje ndio aliolone hilo.
ReplyDeleteMimi naamini mambo mengine yanahitaji tuu common 'sense'..hivi kwa mfano, kujua kuwa ukuaji wa idadi ya watu visiwani haundeni na rasilimali tulizo nazo ikiwa ni pamoja na ardhi..kweli inahitaji degree ua kumsubiri mzungu?
Tukija katika sera yenyewe, sidhani kama tunahitaji tume ya kupoteza fedha na muda ni suala tu la serikali, kutathimini na kupima ardhi yote ya visiwani kama ifuatavyo;
Kwanza, maeneo yote yenye rutuba ni kwa ajili ya kilimo tuu na hayataruhusiwa kuuzwa viwanja.
hata kama mmiliki ataamua kuuza, mnunuzi anunue kwa ajili yakilimo.
Pili, maeneo yote ya uwanda na yasiyo na rutuba yawe ndio ya makaazi.
Tatu, maeneo yote ya fukwe na uwanda wa bahari wapewe wawekezaji kwa iajili ya shughuli za kitalii.
Serikali inunue ardhi kutoka kwa wananchi wanaouza na baadae waipime viwanja ili kuviuza rasmi kwa wanaohitaji.
Serikali ni lazima iwe na maeneo yake ya hakiba ili ukitokea mradi wowote wa maendeleo yatumike na sio kuanza kuvunjia watu na kuwalipa fidia.